Taarifa iliyotolewa Geneva, Uswisi leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR imesema uamuzi huo umetolewa leo na Jopo la Majaji wa Mahakama ya ICC, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kesi kutolewa hukumu katika hali iliyowasilishwa kwa mahakama hiyo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hukumu hii imekuja wakati ambapo makosa sawa ya ukatili yanaendelea kuripotiwa tena katika jimbo la Darfur na maeneo mengine ya Sudan, kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF).

“Kumhukumu Ali Kushayb ni hatua muhimu ya kutambua mateso makubwa waliyopitia waathirika wa uhalifu wake wa kikatili, na ni mwanzo wa haki iliyosubiriwa kwa muda mrefu kwao na familia zao,” amesema Türk.

Ujumbe kwa wanaotenda uhalifu

Kamishna huyo alisifu ujasiri wa waathirika waliotoa ushuhuda wao licha ya maumivu makubwa, wakitumaini kwamba siku moja wahusika wangewajibishwa.

“Ni matumaini yangu makubwa kwamba hukumu ya leo itakuwa ukumbusho mpya kwa wale wanaotekeleza uhalifu wa leo kwamba hakuna atakayesalimika kwa makosa makubwa dhidi ya raia. Watajua kwamba nao watakabiliwa na haki kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria,” aliongeza.

Türk amesema uamuzi huo unathibitisha umuhimu wa ICC kama mahakama ya mwisho ya kutoa haki pale ambapo hakuna uwezekano wa uwajibikaji katika ngazi ya kitaifa, na kwamba mahakama hiyo inabaki kuwa ngome muhimu dhidi ya kutowajibika kwa wahalifu wa vita.

Ali Kushayb ni nani?

Ali Kushayb, aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa makundi ya wanamgambo wa Janjaweed katika eneo la Darfur Magharibi.

Ametiwa hatiani na jopo la majaji watatu mjini The Hague nchini Uholanzi, kwa makosa ikiwemo ubakaji kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, pamoja na ubaguzi wa kisiasa, kikabila na kijinsia.

Hukumu hiyo bado inaweza kukatiwa rufaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *