
Duru ya kwanza ya mazungumzo kuhusu Gaza kati ya Hamas na Israel imemalizika siku ya Jumatatu usiku. “Mazungumzo kwa ujumla yalikuwa mazuri,” vimesema vyanzo vilivyo karibu na wapatanishi wa Misri na Hamas.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Mazungumzo yalikuwa mazuri” kulingana na wapatanishi wa Misri, pamoja na vyanzo vya Hamas vilivyozungumza na idhaa ya Qatar ya al-Jazeera, ambayo iko karibu sana na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas, anaripoti mwandishi wetu huko Cairo, Alexandre Buccianti. “Mazungumzo yalikuwa mazuri jana usiku, na kikao cha kwanza kilichukua saa nne,” kilmesema moja ya vyanzo hivyo. “Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yamepangwa kuanza tena saa sita mchana,” chanzo hicho kimeongeza.
Hata rais wa Marekani Donald Trump amepongeza. “Nadhani mazungymzo yanaendelea vizuri sana, na nadhani Hamas imekubali baadhi ya mambo muhimu sana,” rais wa Marekani amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval. “Tutakuwa na makubaliano kuhusu Gaza, nina uhakika nayo,” ameongeza. Rais huyo kutoka chama cha Republican, mwenye umri wa miaka 79, hata hivyo, amebainisha kwamba ana “mistari nyekundu” kwa majadiliano yanayoendelea, bila kutaja ni ipi.
Mazungumzo haya yasiyo ya moja kwa moja, yanayofanyika Sharm el-Sheikh kwenye mwambao wa Bahari ya Shamu, yanatokana na mpango wa pointi 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump mwishoni mwa mwezi Septemba kuwaachilia mateka wa Israel wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza kwa kubadilishana na Wapalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel, kuandaa zoezi la kuondoka kwa jeshi la Israel hatua kwa hatua kutoka Ukanda wa Gaza na kuwasili kwa msaada wa kibinadamu.
Kulingana na wapatanishi hao, mazungumzo hayo yatadumu kwa siku kadhaa. Leo Jumanne mazungumzo yataendelea kuangazia masuala ya kiufundi. Iwapo maendeleo yatapatikana, mkuu wa ujumbe wa Israel, Ron Dermer, Waziri wa Masuala ya Mikakati wa Israel, na Steve Witkoff, mjumbe wa Rais Donald Trump wa Mashariki ya Kati, watajiunga na mazungumzo hayo.
Wakati huo huo, mashambulizi ya mabomu yanaendelea huko Gaza.
Kwa mujibu wa al-Jazeera, Hamas ilionyesha kuwa kuendelea kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza ni kikwazo cha kuachiliwa kwa mateka. Jana, Jumatatu, milio ya risasi iliendelea kusikika, ingawa, kulingana na wakaazi wa eneo hilo, taifa la Kiyahudi limepunguza mashambulizi yake, linaripoti shirika la habari la Reuters. Mamlaka ya afya ya Gaza iliripoti watu 19 waliouawa katika mashambulizi ya Israel katika saa 24 zilizopita, karibu theluthi moja ya vifo vya kawaida vya kila siku katika wiki za hivi karibuni.
Wakati huo huo katika kumbukumbu ya miaka miwili tangu mauaji ya Oktoba 7 yaliyofanywa na kundi la Hamas nchini Israel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Hamas na Israel kusitisha vita vya Gaza mara moja. Akisema pendekezo jipya la Rais Trump linatoa fursa ya kumaliza mgogoro huo. Aidha katika kipindi cha kumbukumbu hiyo pia Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameonya kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.