Uchunguzi baada ya uchunguzi unaonyesha hali moja inayoendelea: Waisraeli na Wapalestina wengi wamepoteza imani kwa kila upande, na sambamba na hilo, matumaini kwamba siku moja mzozo wao unaweza kumalizika kwa njia ya amani.

Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kiebrania mjini Jerusalemu mnamo Agosti ulionyesha kiwango kikubwa cha uhasama. Asilimia 62 ya Waisraeli waliohojiwa walikubaliana na kauli kwamba “hakuna wasio na hatia huko Gaza.” Miongoni mwa Wayahudi wa Israeli pekee, idadi hiyo ilipanda hadi asilimia 76.

“Nimehuzunishwa na ukosefu wa utu”

“Jambo linalonishtua zaidi kuhusu Israeli ni kutoweka kwa huruma,” anasema Corey Gil-Shuster, mkuu wa programu ya Uzamili ya Utatuzi wa Migogoro na Upatanishi katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv. “Watu hawana hata huruma kwa watoto, wazee au wagonjwa – kama vile wagonjwa wa saratani,” aliambia DW kwa huzuni.

Tangu mwaka 2012, Gil-Shuster amekuwa akiongoza mfululizo wa video mtandaoni unaoitwa The Ask Project, akizungumzia mada nyeti kwa kuwauliza raia maswali ya moja kwa moja mitaani – Waisraeli na Wapalestina.

Katika video moja aliwauliza Wapalestina kama wanaunga mkono mashambulizi zaidi kama lile la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israeli; katika nyingine, aliwauliza Waisraeli kama wanafurahia mateso ya watu wa Gaza.

Masaibu yasiyoisha kwa watu wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Anasema kuwa katika mahojiano ya hivi karibuni kaskazini mwa Israeli, alipomuuliza mwanamke kuhusu huruma kwa watoto na wagonjwa, alijibu tu kwa kuinua mabega.

“Sifikirii hata kuhusu kile dunia inachotufikiria – kinachonitia hofu ni kile kinachotokea ndani yetu. Nimehuzunishwa na jinsi utu ulivyopotea katika mjadala huu,” anasema Gil-Shuster.

“Kutowajali wanadamu” baada ya Oktoba 7, 2023

Mtazamo huo unafanana na wa Khalil Shikaki, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Sera na Maoni ya Umma cha Kipalestina (PCPSR) mjini Ramallah.

“Katika miaka miwili iliyopita kumekuwepo karibu na kutowajali kabisa ubinadamu: jamii zote mbili zimefikia hatua ya kukataa kutambua utu wa upande mwingine,” anasema.

Shikaki anasema hali hiyo imeathiri pia utayari wa watu kukubali suluhu za maelewano kwa ajili ya amani. Katika utafiti wake wa Mei 2025, asilimia 69 ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza na asilimia 88 ya wale wa Ukingo wa Magharibi hawakuamini kuwa Israeli ingeondoka Gaza iwapo Hamas ingesalimisha silaha zake.

Hata hivyo, anaamini kuwa imani sio lazima iwe sharti la awali kwa mchakato wa maridhiano: “Tukisubiri hadi Wapalestina na Waisraeli waaminiane kabla ya kuanza mazungumzo ya amani, hilo halitatokea kamwe,” anasema Shikaki.

UN: Suluhu ya mzozo wa Gaza ni mataifa mawili

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mikakati ya kurudisha maridhiano

Lakini maridhiano yanaweza kuanzia wapi baada ya miongo ya umwagaji damu? Gary Mason, kutoka Ireland ya Kaskazini, anaona uzoefu wa nchi yake kama mfano.

Kupitia shirika lake Rethinking Conflict, Mason anashirikisha uzoefu wa amani wa Ireland ya Kaskazini na watu wa Mashariki ya Kati. “Katika pande zote mbili, matatizo ni yale yale – ardhi, utambulisho na dini,” anasema Mason.

Anasema Waisraeli na Wapalestina, mbali na misimamo mikali, wote wanatamani suluhisho la kudumu. “Iwapo kutapatikana usitishaji wa mapigano katika miezi sita ijayo, bado inaweza kuchukua miaka mitano au kumi kufikia makubaliano kamili ya amani.

Hata sisi Ireland ya Kaskazini, miaka 27 baada ya Mkataba wa Ijumaa Kuu, bado tunaendelea na kazi ya amani,” anaeleza.

“Amani inahitaji uongozi imara”

Kwa mujibu wa Gil-Shuster, wengi katika pande zote mbili tayari wamezoea hali ya vita. Lakini anasema mabadiliko yanaweza kuja kupitia mawasiliano ya kisiasa yenye matumaini.

“Hatua ya kwanza ni kampeni ya mawasiliano: kusema wazi, ‘tumechoka, hatutaki kuendelea hivi, sasa tunataka mabadiliko.’ Watu wanapaswa kupewa maono – kisha ujumbe huo uendelee kuzungumzwa, kuuzwa kama bidhaa,” anashauri.

Mwishoni mwa Septemba, Rais wa Marekani Donald Trump alizindua mpango wa hatua 20 kwa ajili ya amani ya Gaza, akiahidi kusimamisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote. Kamati ya kimataifa inayoongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair imepewa jukumu la kufuatilia utekelezaji wake.

Kwanini Israel inayashambulia majengo Gaza City?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Lakini ndani ya Israeli na maeneo ya Palestina, imani kwa viongozi wao imeporomoka. Waisraeli wachache tu wanaunga mkono serikali ya Benjamin Netanyahu, huku Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akikabiliwa na upungufu mkubwa wa uhalali, kwani hakuna uchaguzi uliofanyika tangu mwaka 2006. Utafiti wa PCPSR unaonyesha asilimia 81 ya Wapalestina wanamtaka aachie madaraka.

Suluhisho la mataifa mawili – ndoto ya mbali?

Shikaki anaamini kuwa uungaji mkono wa nje ni muhimu kuanzisha tena mchakato wa amani. “Marekani kama mshirika mkuu wa Israeli, na nchi za Kiarabu kama watetezi wa Wapalestina, lazima zisaidie kuanzisha upya mazungumzo yenye matumaini,” anasema.

Kulingana na tafiti za pamoja za Israeli na Palestina, Waisraeli wengi wangeweza kubadilisha mitazamo yao endapo kungekuwa na dhamira ya kimataifa thabiti kuelekea suluhisho la mataifa mawili. Kwa upande wa Wapalestina, wazo hilo linapata uungwaji mkono upya – ingawa takribani theluthi mbili bado wanaliona kuwa gumu kutekelezeka.

Mwezi Septemba, Ufaransa, Uingereza, Australia na nchi nyingine zilichukua hatua ya kuitambua Palestina, hatua iliyokuwa zaidi ya ishara ya kisiasa. Mpango wa Trump unataja “njia ya kuaminika kuelekea kujitawala na kuunda taifa la Palestina.”

Oktoba 7: Jinsi shambulio la Hamas lilivyofanyika

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Lakini serikali ya Israeli inaendelea kukataa wazo la taifa la Palestina lenye mamlaka kamili, na badala yake imeongeza kasi ya ujenzi wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Utafiti wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv wa Aprili/Mei 2025 unaonyesha ni asilimia 21 pekee ya Wayahudi wa Israeli wanaounga mkono suluhisho la mataifa mawili.

Maridhiano licha ya mgawanyiko wa maeneo

Kwa wengi, Ukingo wa Magharibi umevunjwavunjwa kiasi kwamba taifa la Palestina linalounganika kijiografia linaonekana kutowezekana. Lakini mfano wa Ireland ya Kaskazini unaonyesha kuwa hata jamii zilizotengwa kimwili zinaweza kujenga uhusiano mpya.

Mason anakumbusha kuwa hata leo mjini Belfast, baadhi ya maeneo ya Waprotestanti na Wakatoliki bado yametenganishwa kwa kuta ambazo hufungwa kila jioni. “Ni kama blanketi la faraja,” anasema. “Wakati utakapofika, zitabomolewa. Miaka 27 baada ya makubaliano, bado ni muda mfupi ukilinganisha na uzito wa kumbukumbu.”

Kwa mtazamo wake, ikiwa Ireland ya Kaskazini – iliyowahi kuchukuliwa kuwa mzozo usiotatuliwa – iliweza kupata amani ya kudumu, basi hata Mashariki ya Kati inaweza kuona siku ya maridhiano. Swali pekee ni: je, pande hizi mbili bado zinaweza kuamini tena katika ubinadamu?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *