Ni katika ukumbi wa mikutano wa ECOSOC, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, ambapo wageni wamekusanyika kushuhudia hafla maalum ya utoaji wa tuzo ya tatu ya Muonesha Njia maarufu kama Trailblazer Award.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, ndiye aliyemkabidhi tuzo hiyo Olukemi Ibikunle, afisa wa magereza kutoka Nigeria anayehudumu katika ujumbe wa MONUSCO, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akipokea tuzo hiyo, Olukemi amesema

“Ni heshima kubwa kupokea tuzo hii, na ni zaidi ya tuzo ni ushahidi kwamba wanawake tunaweza kuwa na ndoto na tukazitimiza.”

Olukemi Ibikunle anasimamia ujenzi wa gereza mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

© MONUSCO

Olukemi Ibikunle anasimamia ujenzi wa gereza mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza na UN News kuhusu uamuzi wake wa kufanya kazi katika operesheni za kulinda amani, amesema:

“Niliamua kufanyakazi katika ulinzi wa amani kwa sababu nilitaka kuchangia uzoefu wangu katika operesheni za amani. Kabla ya kujiunga na operesheni hizi, nilikuwa na uzoefu wa miaka 10 nikifanya kazi nyumbani katika masuala ya magereza, hasa katika urekebeshaji wa wafungwa ili wajiunge tena na jamii.”

Kazi ya Olukemi ndani ya MONUSCO imejikita katika kuboresha usimamizi wa magereza, kutoa mafunzo na ushauri kwa maafisa wa ndani, na kuimarisha shughuli za urekebishaji wa wafungwa  kazi ngumu katika mazingira yenye changamoto.

Olukemi anasema “Kuletwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani nimeweza kuchangia ujuzi wangu, uzoefu wangu kuboresha hali za magereza nchini DRC. Pia nataka kuimarisha mradi wa biogesi katika gereza la Uvira, Mashariki mwa DRC.”

Kwa Olukemi, heshima hii si yake binafsi tu. Anaongeza “Wanawake wanaweza kuleta mabadiliko, hivyo nilijitoa kimasomaso ili kuwaonesha wanawake wengine kwamba tunaweza kuleta mabadiliko.”

Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed anazungumza katika hafla ya 2025 ya Tuzo ya Maofisa wa Haki na Marekebisho Wanawake.

UN Photo/Evan Schneider

Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed anazungumza katika hafla ya 2025 ya Tuzo ya Maofisa wa Haki na Marekebisho Wanawake.

Hadithi yake inaangazia kazi muhimu lakini mara nyingi isiyotambulika ya maafisa wa magereza katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa  kazi ya kulinda haki, utu, na heshima za binadamu katika mazingira tete.

Tuzo ya Muonesha Njia ilianzishwa kutambua wanawake wanaoonesha uongozi, ubunifu na kujitolea katika kazi za magereza na haki.
Mwaka huu, Olukemi Ibikunle amejiunga na safu ya wanawake mashujaa wanaothibitisha kwamba ujasiri, kujitolea, na huruma ndizo silaha halisi za kudumisha amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *