Lengo namba 2 kati ya malengo 17 ya Maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa linataka kutokomeza njaa na kuhakikisha kuna uhakika wa chakula tena kilicho bora pamoja na kukuza kilimo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Kwa kutambua kaunti ya Samburu ina hali ya Ukame, Gavana wa kaunti hiyo kwa kushirikiana na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo ni la Mpango wa Maendeleo UNDP, la wanawake UN Women na la watoto UNICEF waliketi chini na wananchi wa kaunti ya Samburu na baada ya majadiliano wakakubaliana kuanzisha mradi wa kutoa mbegu zinazohimili hali ya ukame pamoja na mifugo ambayo inahimili ukame na inatoa maziwa kama ngome aina ya Sahiwal.

Mradi huo umeleta manufaa makubwa kama anavyoeleza kijana Juma Leodip mnufaika wa mifugo.

“Tulikuwa tumeingia watu wote wa Lukurroto tukaongea na tukakubaliana kutoa ng’ombe kwa vijana, wamama wajane, wale wasio na uwezo pamoja na walemavu. Mimi nilipewa ngombe katika kundi la vijana. Nilivyopewa alikuwa mdogo sana, wakati naendelea kumpatia malisho nikaona huyu ngombe yupo na utofauti sababu ana nyama na pia ana maziwa na tena nikipeleka hayo maziwa kuuza sokoni nitapata pesa nikaona huyu ngombe ataweza kunifaidisha kwa haraka. Naona kaunti wanafanya kazi nzuri, vile vitu vyote wanaleta vinakuwa na faida sasa mimi nipo na furaha sana nashukuru serikali yetu sababu wamefanya kitu cha maana zaidi.”

Mnufaika mwingine ni Rende Lucia

“Nilipata mbegu na ngombe, hii mbegu ni nzuri kwasababu imezaa vizuri na hiyo ngombe ana nyama na maziwa. Tangu nianze kutumia hii mbegu mimea imekuwa ikitoa chakula kizuri na inapambana na wadudu wengi. Chakula ninachovuna kingine naweka na kingine nauza ili kupata fecha ya kusomesha watoto wangu. Ngombe wangu pia amekuwa na kuzaa na sasa napata maziwa asubuhi na jioni.”

Mbali na kaunti ya Samburu, mradi huu unatekelezwa katika kaunti nane nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *