Katika taarifa yake iliyotolea mjini New York Marekani Jumatino suiku Katibu Mkuu António Guterres “amezitaka pande zote zinazohusika kuheshimu kikamilifu masharti ya makubaliano hayo, ikiwemo kuachiliwa kwa heshima kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza kwa zaidi ya miaka miwili.”

Rais Donald Trump alitangaza kupitia mitandao ya kijamii Jumatano usiku kwamba Hamas imekubali kuwaachilia huru mateka wote walioko Gaza “Hivi karibuni kabisa, huku Israel ikikubali kuanza kuondoa vikosi vyake vya ardhini hatua kwa hatua hadi mstari ulioafikiwa.”

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari zikiinukuu Qatar, makubaliano hayo yanahusisha “masharti na taratibu za utekelezaji wa awamu ya kwanza itakayomaliza vita, kuachiliwa kwa mateka wa Kiyahudi na wafungwa wa Kipalestina, na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.”

Wapalestina Gaza wanasherehekea tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano.

Wapalestina Gaza wanasherehekea tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano.

Sifa kwa wapigania amani

“Nakaribisha tangazo la kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza, kulingana na pendekezo lililowasilishwa na Rais Donald J. Trump,” Guterres amesema katika taarifa yake.

Ameongeza kuwa “Naipongeza juhudi za kidiplomasia za Marekani, Qatar, Misri na Uturuki ambazo zimefanikisha hatua hii muhimu sana.”

Bwana Guterres amesisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa usitishaji mapigano wa kudumu.

Kulingana na mpango wa Marekani, Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Hilali Nyekundu utasimamia uingizaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

“Ni lazima kuruhusu mara moja na bila vizuizi misafara ya misaada yenye bidhaa muhimu na biashara kuingia Gaza. Mateso haya lazima yakome,” amesema Katibu Mkuu, akiahidi kuwa Umoja wa Mataifa utasaidia kutekeleza makubaliano hayo na kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu, pamoja na juhudi za uokoaji na ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *