London, England. Nyota wa zamani wa Ligi Kuu ya England, Ivan Klasnic, amesema kuwa anaweza kufariki wakati wowote baada ya afya yake kudhoofu kutokana na dawa za kutuliza maumivu alizopewa na klabu yake ya zamani bila kufahamu kuwa tayari alikuwa na tatizo la figo.
Klasnic, ambaye tayari amefanyiwa upandikizaji wa figo mara tatu, alipata fidia ya pauni 4 milioni kutoka kwa klabu yake ya zamani ya Werder Bremen mnamo mwaka 2020 baada ya kuthibitika kuwa dawa walizompa zilichangia kuongezeka kwa ugonjwa wake wa figo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 45, anayefahamika zaidi nchini England kwa kuchezea klabu ya Bolton kwa miaka minne, alizungumza kuhusu hali yake ya kiafya kwenye televisheni ya Ujerumani juzi.
Katika mazungumzo yake, raia huyo wa Croatia alisema:
“Nani ajuaye nina muda gani wa kuishi. Inabidi nishukuru kwamba bado niko hai, ingawa ni mgonjwa na nahitaji kutumia dawa kila siku. Kwa kweli nimekasirika. Sitamani mtu yeyote apitie mateso niliyopitia. Haijalishi nimepokea fidia kiasi gani, afya yangu haitarudi tena kama ilivyokuwa, ninakufa.”
“Ni vigumu kucheza bila kutumia dawa za kutuliza maumivu kama unataka kufanya vizuri uwanjani. Sidhani kama kuna mtu anaweza kucheza michezo ya kulipwa bila kutumia dawa hizo. Lakini kama ningejua kwamba nina matatizo ya figo, nisingekubali kutumia dawa hizo.”
Klasnic alichezea Werder Bremen kati ya mwaka 2001 na 2008. Mwaka 2007 figo yake ilifeli na alihitaji kupandikizwa figo kwa mara ya kwanza, jambo lililomweka nje kwa miezi 10.
Mwaka uliofuata, Klasnic alidai kuwa madaktari wa klabu hiyo walikuwa tayari wanajua kuhusu tatizo hilo tangu mwaka 2002 na akaanzisha kesi dhidi yao.
Madaktari wawili waliokuwa wakifanya kazi kwa niaba ya klabu walipatikana na hatia. Kwa mujibu wa BMJ, madaktari hao Götz Dimanski, aliyekuwa daktari wa timu mwaka 2007 na Manju Guha, daktari wa moyo aliyekuwa akifanya uchunguzi kila mwaka waliamriwa kulipia gharama za matibabu ya zamani na zijazo za Klasnic pamoja na fidia ya kupoteza kipato.
Klasnic alisema pia kuwa hiyo ndiyo sababu iliyomfanya aondoke klabuni alipomaliza mkataba wake, kwani hakutaka tena kufanya kazi na madaktari hao.
Baada ya kuondoka Bremen, Klasnic alijiunga na Bolton mwaka 2009, ambapo alifunga mabao 24 katika mechi 93 alizocheza. Wakati anajiunga na Bolton, tayari alikuwa amefanyiwa upandikizaji wa figo mara mbili. Alipata upandikizaji wa tatu mwaka 2016, baada ya kuugua tena.
Awali, alipata fidia ya pauni 900,000, lakini mawakili wake walipeleka kesi hiyo mahakama ya juu zaidi nchini Ujerumani, na Klasnic alishinda fidia ya ziada ya pauni milioni 3.6, na kufanya jumla ya fidia aliyopata kuwa zaidi ya pauni 4 milioni.
Hata hivyo, fedha hizo hazilinganishwi na afya njema. Wakili wake, Matthias Teichner, alisema:
“Hakuna kiasi cha fedha kinachoweza kufidia madhara makubwa na ya kudumu kwa afya ya mteja wangu, lakini fidia hii ni hatua nzuri ya kutoa hisia ya haki. Kwa angalau, madaktari sasa wako tayari kuonyesha majuto yao kuhusu tukio hili, jambo ambalo kwa maoni yangu lilichelewa sana.”
Klasnic aliondoka Bolton baada ya kushuka daraja mwaka 2012, kisha akajiunga kwa muda mfupi na Mainz ambapo alistaafu mwaka 2013.
Katika kipindi chake Bremen, alitwaa ubingwa wa ligi na kombe la taifa. Pia aliichezea timu ya taifa ya Croatia mara 41, akifunga mabao 12. timu nyingine ambazo alifanikiwa kuzitumikia ni Nates na ST Paul ambayo alianzia soka lake.