SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati yake ya Uchaguzi limetangaza orodha ya awali ya wagombea waliorejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ambapo mchakato wa usaili unatarajiwa kufanyika Oktoba 15, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Benjamin Kalume, wagombea hao wanatoka katika makundi tofauti ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wawakilishi wa klabu

Kwa upande wa nafasi ya mwenyekiti wa Bodi majina matatu yametajwa kutaka kurithi nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Steven Mnguto  aliyejiuzulu Juni 14, mwaka huu.

Wanaotaka kumrithi Mnguto ni pamoja na Nassor Idrissa Muhamed, Said Suud Said na Hoseah Hopaje Lugano. 

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kamati hiyo imeorodhesha wagombea wawili ambao ni Kheri Nassor Missinga na Hassan Ramadhan Muhsin ambao watachuana kuwania nafasi hiyo muhimu ya kusaidiana na mwenyekiti katika uendeshaji wa shughuli za ligi.

Kwa wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu, majina mawili yametajwa ambayo ni Japhet Mboto Makau na Gilbert Morice Nkoronko.

Katika kundi la Championship wawakilishi waliorejesha fomu ni Hillary John Ndumbaro na Ahmed Waziri Gao. 

Kwa upande wa First League, jina pekee lililotajwa ni la Azimkhan Akber, ambaye atakuwa mwakilishi wa ligi hiyo ya daraja la tatu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *