Serengeti. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewaeleza wananchi wa Wilaya ya Serengeti umuhimu wa kuchagua viongozi kwa kuzingatia weledi na sio jinsia zao huku akieleza namna yeye kama mwanamke alivyoweza kuliongoza taifa kwa miaka minne na kufanya makubwa.
Mgombea huyo ameyasema hayo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 wakati akihutubia mkutano wa mwisho wa kampeni katika Mkoa wa Mara, uliofanyika eneo la Mugumu, wilayani Serengeti kabla kuelekea kwenye mkutano mwingine, Bariadi Mjini mkoani Simiyu.
Amesema alipoingia madarakani, kuna waliobeza kuwa hataweza lakini sasa yanazungumzwa mengine.
Samia ameeleza kuwa wapo wanaosema mila na desturi zao hazitaki mwanamke kugombea, hivyo kutumia fursa hiyo kutoa elimu na umuhimu wa mshikamano wa Watazania (wanaume na wanawake) na katika kuleta maendeleo kwa familia au taifa na kuwa kwenye maendeleo hakuna mwanamke au mwanaume.
Mgombea huyo alianza kwa kueleza kuwa mshikamano wa Watanzania ni muhimu na kuwa pamoja na mila na desturi zilizopo, suala la umoja wa Watanzania ni suala muhimu.
“Mungu alivyotuumba hakuumba kwamba mwenye kichwa fulani anachozaliwa nacho ana akili zaidi kuliko mwingine, lakini pia hatukuambiwa kwamba mwanamke ana akili zaidi kuliko mwanaume au mwanaume ana akili zaidi kuliko mwanamke.
“Mwenyezi Mungu alitutofautisha kwenye zile kazi alizotupa kazi ambazo alituambia wanawake tutabeba mimba na tutazaa kwa uchungu na akatuumba kwenye maumbile hayo,” amesema na kuongeza:
“Wanaume mkaambiwa ninyi ni wasimamizi wa wanawake na mtafanya kazi kutunza familia zenu, lakini jinsi tunavyokwenda wanawake nao sasa wanafanya kazi na kutunza familia zao.”
Amesisitiza kwamba: “Kwenye maendeleo hakuna mwanamke, hakuna mwanaume, mimi ninayesema hapa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndani ya miaka minne nimefanya makubwa sana.
“Sasa ingekuwa mwanamke hawezi nisingeweza kuyafanya Mungu alituumba wote na akili sawa na akatupa na uwezo wa kufikiri, ukiwa mwanamke unafikiri, ukiwa mwanaume unafikiri,” amefafanua.
Mgombea huyo amesema kuwa mwanamke ni mwanimifu zaidi na mtendaji zaidi kwa sababu ya woga kuliko mwanaume.
“Nataka niwaambie ndugu zangu, niwaambie wazee wetu pamoja na mila na desturi zetu na nimeanza kusikia maneno kwamba huko CCM Mara sisi wametupa wagombea wanne wanawake kwani wanawake wana nini?” amehoji.
Mgombea huyo amesema Tanzania hii itaendelezwa na itejengwa na wanaume na wanawake wote kwa umoja wao, cha muhimu ni wote kushikamana kama waasisi wetu walivyotuambia tushikamane tujenge nchi yetu kwamba huyu mwanamke huyu mwanaume hayo hayapo,” amesema.
Samia amesema ulimwengu kwa sasa unajengwa na wanaume na wanawake na kuwa kuna wanasayansi, madaktari wanaume na wanawake.
“Unapokwenda hospitalini husemi huyu daktari ni mwanamke asinitibu, unapolindwa na ulinzi na askari mwanamke hawafai kulinda? Si wanapangiwa malindo na Tanzania yetu iko salama, tofauti iko wapi?” amehoji Samia.
“Niwaombe ndugu zangu mila, desturi na makabila hayatatusaidia sana kwenye mwendelezo wa nchi yetu niwaombe tuimariahs mshikamano. Hata mimi jilipoingia kuna waliobeza kwamba sitaweza lakini leo tunazungumza mengine.
Mkoa wa Mara una wagombea wanawake wane, wagombea hao na majimbo yao kwenye mabano ni Esther Matiko (Tarime Mjini), Esther Bulaya (Bunda mjini), Mgore Kigera (Musoma mjini) na Mary Daniel (Serengeti).
Mgombea huyo aliwaomba wananchi hao kuichagua CCM ili kuendeleza mkakati wa kuufanya mji wa Mugumu kuwa kitovu cha utalii kwa mkoa wa Mara kutokana fursa zilizopo za uwekezaji na ukaribu wa hifadhi ya Serengeti na kuwa mji wa Mugumi ni wa mkakati kiutalii.
Amesema Mugumu ni miongoni mwa miji yenye umuhimu wa fursa za uwekezaji ikiwemo hoteli za utalii kwa kuwa upo katikati ya maeneo ya hifadhi kwa wageni wanaotoka Sirari na Seronera kwenda Kogatende kaskazini mwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako pia kuna utalii wa mzunguko wa nyumbu wanaohama kwenye ikolojia ya Serengeti.
“Kipindi hiki tumeshuhudia uwekezaji kwenye sekta ya utalii hapa Mugumu na wawekezaji wanavutiwa na vitu vingi ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa mipango ya kutunza na kuendeleza hifadhi. Mipango ambayo imewezesha kutunza na kuendeleza hifadhi mipango ambayo imewezesha mara kadhaa mbuga yetu ya Serengeti kushinda tuzo za kimataifa,” amesema.