Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 19 kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, vyama vya siasa vinaendelea kufanya kampeni katika maeneo mbalimbali nchini huku mambo manne yakitawala mjadala kwa wananchi.

Baadhi ya matukio ya kisiasa ya ndani na nje ya nchi, yamekuwa gumzo kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali kama vile mitandao ya kijamii, majukwaa ya wanaharakati pamoja na jumuiya ya kimataifa.

Hata hivyo, kutokana na baadhi ya matukio hayo kuhusisha jinai, wananchi wamehimizwa kulinda amani, utulivu na umoja hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ili taifa liendelee kuwa moja na lenye utulivu.

Uchaguzi mkuu

Kwa kuwa hiki ni kipindi cha uchaguzi, mjadala mkubwa umekuwa ni kuhusu uchaguzi huo huku vyama vya siasa vikiwa na misimamo tofauti kuelekea siku ya uchaguzi huo, wananchi nao wakiwa na mitazamo tofauti.

Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wafuasi wake, kimekuwa kikitumia kaulimbiu ya “Oktoba Tunatiki”, kikihamasisha wananchi kwenda kukipigia kura siku ya uchaguzi ili kiendelee kuiongoza Serikali.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama,mkoani Mara wakiwa katika uwanja wa Mwenge wilayani humo wakisubiri kuanza kwa mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM,Samia Suluhu Hassan,leo Ijumaa Oktoba 10,2025

Chama hicho kinahamasisha wananchi kuwapuuza wote wenye lengo la kuharibu amani na utulivu kwani hawana nia njema na maisha yao. Viongozi wake wanasisitiza wajitokeze kwenda kupiga kura ili wawachague viongozi wanaowataka hasa wanaotokana na chama hicho.

Wakati CCM kikitoa hamasa hiyo, baadhi ya wanaharakati wasiokubaliana na uchaguzi mkuu ujao, wanaibua mjadala mitandaoni huku wakieleza kwanini taifa linahitaji mabadiliko ya Katiba itakayoruhusu Tume huru ya uchaguzi.

Mbali na hao, ACT Wazalendo kinahamasisha wananchi kulinda kura zao baada ya kupiga kura ili wasiibiwe kura zao, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za uchaguzi ambazo zinaelekeza wananchi kukaa umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.

Kesi ya Lissu

Kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ni miongozi mwa mambo yanayojadiliwa na wananchi kutokana na mwendeo wa kesi yenyewe, akishitakiwa kwa makosa ya uhaini na uchochezi.

Lissu alikamatwa Aprili 2025 Mbinga mkoani Ruvuma alikokwenda kuelimisha wananchi kuhusu msimamo wa chama chake wa “No reforms, no election” (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) ikiwa ni njia ya kuzuia uchaguzi huo hadi mabadiliko ya msingi yatakapofanyika.

Mabadiliko ambayo Chadema wanayataka ni kuwa na mfumo wa uchaguzi ambao utatoa nafasi sawa kwa vyama vyote kushindana kwa haki na wananchi kuchagua viongozi wanaowataka na siyo kulazimishwa au kuwekewa viongozi.

Shauri hilo dhidi yake, lilianzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania na sasa hatua inayoendelea ni usikilizaji wa mashahidi wa upande wa Jamhuri ambapo tayari wawili wametoa ushahidi wao.

Watanzania wamekuwa wakifuatilia shauri la mwanasiasa huyo huku wakiwa na mitazamo tofauti. Wanaharakati nao wanasisitiza kwamba haki itendeke kwenye kesi hiyo inayomkabili Lissu—mwanasheria mbobevu aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS).

Kutekwa kwa Polepole

Oktoba 7, 2025, mkosoaji wa Serikali ya Tanzania, Humphrey Polepole alichukuliwa nyumbani kwake na watu ambao hawajatambuliwa na hasi sasa hajulikani alipo huku Jeshi la Polisi likieleza kufungua jarada la uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati mjadala huo ukipamba moto, familia ya Polepole kupitia kwa mwanasheria wake, Peter Kibatala imefungua shauri Mahakama kuu ikitaka Polepole afikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka rasmi.

Polepole ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba kabla ya kujiuzulu, Julai 13, 2025, hajulikani alipo hadi sasa, jambo ambalo linaibua hofu kuhusu usalama wake, akiwa ni mmoja wa watu waliotoweka katika mazingira kama hayo.

Kada huyo wa CCM amekuwa akizungumza mtandaoni akifichua na kukosoa mambo mbalimbali yaliyofanywa na Serikali huku akieleza kwamba haoni kama kuna uchaguzi nchini kwani uchaguzi ujao “ni kiini macho”.

Vita vya Palestina, Israel

Kwa upande wa kimataifa, mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina huko Gaza, ni jambo linaloibua hisa za wananchi huku baadhi yao wakilaani mauaji yanayofanyika dhidi ya wanawake na watoto.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limefanya mkutano wake hivi karibuni ambapo Mataifa mengi yamepiga kura ya kutaka Palestina kutambuliwa kama Taifa huru ikiwa ndiyo njia ya kumaliza mapigano hayo.

Mataifa ya Uingereza na Ufaransa ambayo awali yaliiunga mkono Israel katika mapigano hayo ya muda mrefu, yamebadili msimamo wao, sasa wanataka kukomeshwa kwa mashambuzi hayo, na wameamua kuitambua rasmi Palestina.

Wachambuzi wafafanua

Mchambuzi wa masuala ya siasa Dk Paul Loisulie amesema suala la Oktoba Tunatiki na Oktoba Tunatoka, kesi ya Lisu na kutekwa kwa Polepole yote mzizi wake ni uchaguzi mkuu.

“Lissu anashtakiwa kwa sababu ya uchaguzi mkuu, Polepole katekwa kwa sababu ya uchaguzi mkuu na hayo mengine yanaangukia kwenye uchaguzi, sasa haya yanatuonyesha kuwa tunahitaji maboresho makubwa katika uchaguzi huu kwa wadau wote kuzungumza lugha moja, kwa sasa watu wamegawanyika,” amesema.

Dk Loisulie amesema hayo yote yanatokea kwa sababu watu hawazungumzi lugha moja, jambo ambalo mzizi wa tatizo ni uchaguzi mkuu.

Amesema ili kuondokana na mtego huu wa kila mtu kuongea lugha yake majadiliano ya kitaifa yanahitajika ili kuleta umoja unaopotea.

Kwa upande wake, Wakili Greyson Mgonja amesema suala la uchaguzi lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na litatekelezwa kulingana na sheria zilizopo na hata ambao hawashiriki uchaguzi huo wamefanya hivyo kulingana na sheria.

“Ili kulinda amani ya nchi yetu ni lazima tusimame kwenye sheria, tukienda kinyume na hapo tutavuruga amani ya taifa letu. Suala la Polepole hadi sasa hakuna majibu rasmi kwa sababu tunaambiwa hakuwa Tanzania,” amesema.

Amesema suala la uhalifu ni sehemu ya jamii na hapo watu wanaweza kutumia mwanya huo kuharibu amani ya Tanzania.

Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Elieth Mtaita, kuhusu yanayoendelea kuelekea uchaguzi mkuu, amesema jambo la kawaida katika demokrasia kwa wananchi kuwa na mitazamo tofauti.

Amesema jambo la muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi, na amani bila vitisho, ukandamizaji wa haki za kiraia au matendo ya kulazimisha matokeo.

“Kitendo cha mtu maarufu ‘kutekwa’ au ‘kupotea’ bila maelezo ya wazi ni tishio kwa utawala wa sheria haki ya usalama wa kila raia, awe mwanasiasa au la, ni jambo la msingi katika taifa linalozingatia utawala bora,” amesema.

Amesema suluhu ni kuhakikisha kuna uwazi kutoka vyombo vya usalama na kama kuna makosa, basi yawekwe wazi kisheria, sio kwa vitisho.

“Kufunga au kuzuia sauti za upinzani si suluhisho; badala yake, majibizano ya hoja na uwajibikaji wa kisiasa ndiyo nguzo ya demokrasia ya kweli,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *