
Somalia na Djibouti zimekaribisha makubaliano ya amani yaliyofikiwa kwa ajili ya kusitisitisha vita katika Ukanda wa Gaza na kupongeza juhudi za kikanda na kimataifa za kufanikisha usitishaji vita, kuhahakisha misaada ya kibinadamu inafika Gaza na wafungwa na mateka wote wanaachiwa huru.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilieleza jana katika taarifa yake kuwa inaunga mkono haki za Wapalestina ikiwemo kuasisiwa nchi huru ya Palestina.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa: Somalia inatumai kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo, amani ya kweli itapatikana ili kuhitimisha mateso ya raia wa Palestina na kuimarisha hali ya usalama katika eneo.
Naye Rais Omar Guelleh wa Djibouti amepongeza juhudi za Qatar, Misri, Uturuki na Marekani katika uwanja huo. Amesema makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kikamilifu, misaada ya kibinadamu inapasa kuruhusiwa kuingia Gaza na njia ya kuaminika ya suluhisho la serikali mbili inapasa kupatikana.
Makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yalifikiwa kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) siku ya Alhamisi katika mji wa Sharm el-Sheikh huko Misri, kwa upatanishi wa Qatar, Misri, Marekani na Uturuki.
Mpango huo wenye vipengele 20 wa kusitisha mapigano Gaza, uliotangazwa kwa mara ya kwanza Septemba 29 mwaka huu unajumuisha kuachiwa huru mateka wote wa Israel mkabala wa kuachiwa huru wafungwa wa Kipalestina, kusitisha mashambulizi, kupokonywa silaha Hamas, na kuijenga upya Gaza.