Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema lengo lake kufikia mwaka 2030 ni kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka, ili kuongeza fursa za kiuchumi, ajira, na kuimarisha viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Maswa, mkoani Simiyu, Dkt. Samia amesema serikali imepanga kujenga zaidi ya skimu 700 za umwagiliaji nchi nzima, hatua itakayowasaidia wakulima kulima kwa tija bila kutegemea misimu ya mvua pekee.
Amesema mpango huo ni mwendelezo wa juhudi zilizochochea mafanikio yaliyopatikana kupitia programu za ruzuku za mbolea, chanjo ya mifugo, na upatikanaji wa pembejeo bora, ambavyo vimeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na umeme, huku miradi inayoendelea ikiendelezwa na mingine mipya kuanzishwa ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma kwa ukaribu na kwa wakati.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi