
Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Mshikamano na Watoto na mabarobaro wa Kipalestina, umefanyika leo Jumapili kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Kiislamu mjini Tehran, kwa kuhudhuriwa na maafisa wa ndani, wageni kutoka nchi za nje na wanaharakati wa Kipalestina.
Mkutano huo ambao unafanyika kwa mnasaba wa Kumbukumbu ya Shahidi Muhammad al-Durrah na Watoto Mashahidi wa haza, unachunguza changamoto za Palestina, kwa kushirikisha wawakilishi kutoka Yemen, Lebanon, Pakistan, Afrika Kusini, India, na Algeria, na kutakuwa na tume nne maalum: kisiasa, kisheria, vyombo vya habari, wanawake na watoto.
Ayatullah Mohammad Hassan Akhtari Mkuu wa Kamati ya Kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Wananchi wa Palestina amelaani jinai za utawala wa Kizayuni katika kikao hiki na kuzungumzia suala la utawala huo kutengwa duniani na kutoa wito wa kuweko uungaji mkono wa kimataifa kwa ajili ya ujenzi mpya wa shule na hospitali huko Gaza.
Khaled al-Qadoumi, mwakilishi wa Hamas mjini Tehran ameichukulia Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa kuwa ni hatua ya mabadiliko katika kufichua sura ya utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, muqawama wa Palestina bado una nguvu na unaendelea licha ya zaidi ya mashahidi 76,000 wakiwemo watoto 20,000.
Balozi wa Yemen mjini Tehran Ibrahim al-Dailami, akizungumzia muqawama wa watu wa Palestina, amesema kuwa, jumuiya za kimataifa hazina itibari.
Nasser Abu Sharif, mwakilishi wa Jihadul-Islami ameashiria kupungua uungaji mkono wa kimataifa kwa utawala wa Kizayuni baada ya tarehe 7 Oktoba na kusisitiza ulazima wa kuendeleza jihadi katika nyanja zote.