Liverpool, England. Kocha wa zamani wa Aston Villa, Steven Gerrard amejiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwa kocha mkuu wa Rangers baada ya kuwaambia mabosi wa timu hiyo wakati huu sio sahihi.

Gerrard mwenye umri wa miaka 45, ambaye alishinda taji la Ligi Kuu Scottland akiwa na Rangers mwaka 2021 kabla ya kuhamia Aston Villa, alifanya mazungumzo na mabosi wa timu hiyo, jijini London  waliomtaka kuchukua mikoba ya Russell Martin Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita.

Hata hivyo, kulingana na ripoti za tovuti ya Daily Mail, moja ya masharti aliyotoa ni kusimamia usajili wa wachezaji, lakini baada ya mazungumzo ya muda  Gerrard alimwambia mwenyekiti wa timu hiyo Andrew Cavenagh na makamu wake Paraag Marathe kuwa anataka kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Wawakilishi wa Rangers ambao ni pamoja na  mkurugenzi wa michezo Kevin Thelwell, Mkurugenzi Mtendaji Patrick Stewart na Gretar Steinsson, wameanza kuzungumza na makocha wengine baada ya Gerrard kukataa na sasa kocha wa zamani wa Sheffield Wednesday, Danny Rohl, anaonekana kupewa nafasi kubwa ya kupata ajira.

Familia ya Gerrard bado ipo Bahrain ilipoanza kuishi wakati staa huyu wa zamani wa Liverpool alipopata ajira ya kuifundisha Al-Ettifaq na inaelezwa hiyo ilikuwa sababu moja wapo iliyotia ugumu yeye kukubali kuifundisha timu hiyo.

Rangers inataka kumtangaza kocha wao mpya wakati wa mapumziko ya kimataifa na kabla ya mchezo wa ligi nyumbani dhidi ya Dundee United mwishoni mwa wiki ijayo.

Uamuzi wa Gerrard utakuwa pigo kwa mashabiki wengi wa Rangers waliokuwa wakitamani kumwona akirudi tena kama kocha, baada ya kuwapa mafanikio alipokuwa na kikosi chao miaka minne iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *