
Hali bado bado ni tete nchini Madagascar, wakati Rais Andry Rajoelina haijulikani aliko. Hata hivyo Ofisi ya rais, leo Jumatatu Oktoba 13, kwenye ukurasa wake wa Facebook, imebainisha kwamba rais huyo “atahutubia wananchi wa Madagascar leo saa 1:00 jioni (sawa na 18 saa za Ufaransa). Nchi imekumbwa tangu Septemba 25 na maandamano yaliyokandamizwa kupinga kukatika kwa maji na umeme, hali ambayo imegeuka kuwa maandamano dhidi ya serikali na wito wa kutaka rais Andry Rajoelina ajiuzulu.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Rais wa Madagascar Andry Rajoelina hajazungumza hadharani tangu kikosi cha jeshi (CAPSAT) kitangaze hadharani kuunga mkono maandamano ya raia Jumamosi asubuhi, anaandika mwandishi wetu huko Antananarivo, Guilhem Fabry. Ni Waziri Mkuu wake pekee aliyezungumza Jumamosi jioni kuitisha mazungumzo. Ofisi ya mawasiliano ya rais jana asubuhi ilitoa taarifa ikilaani “jaribio la kunyakua mamlaka kinyume cha sheria na kwa nguvu,” na taarifa nyingine jana usiku, ikiripoti vitisho vya wazi dhidi ya Mkuu wa Nchi.
Rais aonekana kutengwa
Andry Rajoelina anaonekana kutengwa zaidi kuliko hapo awali. Waziri Mkuu wake wa zamani, Christian Ntsay, na mfanyabiashara Mamy Ravatomanga, ambaye alikuwa bado mshirika wa karibu wa rais hadi hivi majuzi, aliwasili Mauritius kwa ndege ya kibinafsi siku ya Jumamosi jioni.
Kabla ya jana Jumapili, CAPSAT ilimteua Mkuu mpya wa Majeshi, Meja Jenerali Pikulas, kuchukua nafasi ya Jenerali Rakotoarivelo, Waziri wa Majeshi aliyeteuliwa hivi karibuni. Lakini kukabidhiwa huku kwa mamlaka hakujaidhinishwa na Andry Rajoelina, ambaye angepaswa kutia saini amri kwa uteuzi huu.
Siku ya Jumapili umati mkubwa wa watu ulikusanyika kwenye eneo maarufu la Mei 13 huko Antananarivo kusherehekea wanajeshi wa CAPSAT. Takriban watu elfu moja walikusanyika katika uwanja huu wa kiishara wa mji mkuu wa Madagascar, kitovu cha maandamano yote maarufu ambayo Madagascar imepitia tangu 1972.
Adhuhuri, magari matatu ya kivita yalipita katikati ya umati. Wanajeshi hao walisimama huku wakitabasamu, wakiwa na silaha mikononi, wakiwasalimia waandamanaji waliowashangilia huku wakipeperusha bendera za Madagascar. Waliokuwepo ni Kanali Randrianirina, ambaye aliongoza uasi, pamoja na rais wa zamani Marc Ravalomanana, aliyepinduliwa na Andry Rajoelina mwaka 2009, na “Mikolo,” mwanafunzi mwenye umri wa miaka 19 ambaye amekuwa ishara ya maandamano ya vuguvugu la vijana la Gen Z nchini Madagascar.