Leo ni Jumamosi 3 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria inayosadifiana na 25 Oktoba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 214 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa nchini Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani. 

Évariste Galois

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, alimu na malenga aliyekuwa na uwezo mkubwa wa Waislamu.  Alizaliwa mwaka 1224 Hijiria mjini Zanjan, moja ya miji ya Iran na akiwa kijana alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya masomo. Akiwa mjini Isfahan alijiunga na chuo cha hauza ambacho kilikuwa moja ya vituo vyenye itibari katika elimu ya kidini wakati huo ambapo alifikia elimu ya juu na kisha kurejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo yake.  Sambamba na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani, aliandika vitabu vingi ambavyo baadhi yake ni ‘Hujjatul-Abraar’ na ‘Hidayatul-Muttaqin’.  

Ayatullah Mirza Abu Abdillah Sheikhul-Islam Zanjani

Miaka 144 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania. Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo. Mchoro wa ‘The Girls of Avignon’ wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni ‘Guernica’. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica. Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973.

Pablo Picasso

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Swadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq.  Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini.  Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Swadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala nchini humo. 

Ayatullah Sayyid Ismail Swadr

Na katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita aliaga dunia Abul Qassim Halat mshairi, mchekeshaji na mtarjumi wa zama hizi wa Kiirani. Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 16 na akaondokea kubobea katika mashairi ya vichekesho. Malenga huyo alikuwa akizifahamu vyema lugha za Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu. Miongoni mwa athari zake muhimu ni tarjama ya maneno yenye thamani kubwa ya Bwana Mtume (saw) na Imam Ali bin Abi Talib (as). Abul Qassim Halat ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa katika uga wa maishairi.

Abul Qassim Halat

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *