Akizungumza mjini  Dar es Salaam, Jenerali Mkunda amesema  Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (TPDF) halitakaa  kimya huku makundi ya waandamanaji yakiingia mitaani, kuvuruga amani na kupinga mchakato halali  unaoendelea wa uchaguzi.

Amesisitiza kwamba jeshi, kwa kushirikiana na polisi na vyombo vingine vya usalama, liko tayari kufanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ili kurejesha utulivu iwapo machafuko yataendelea. Amesema vitendo vinavyoshuhudiwa kwa sasa ni uhalifu unaopaswa kukomeshwa mara moja. 

” Ndugu wananchi, ikumbukwe kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya sheria, ambayo lazima izingatiwe na kuheshimiwa. Kutokana na hali hiyo Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania, linawataka  watu wote wanaojishusisha na vitendo vya kihalifu kuacha vitendo hivyo mara moja, ili kuepusha madhara yasiokuwa ya lazima kwa ustawi wa jamii na taifa letu. Endapo vitendo vya uhalifu vitaendelea , jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania kwa kushirikia ana vyombo vingine vya usalama vitaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ,” alisema Jenerali Mkunda.

Tanzania Arusha 2025 | Uchaguzi wa Tanzania 2025
​​​​​​Kulingana na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International watu kadhaa wameuwawa na wengine kukamatwa tangu vurugu hizi zilipoanza Oktoba 29. Picha: AP Photo/picture alliance

Onyo hilo linakuja huku umma ukidai kutoridhika na mchakato wa uchaguzi, na kushuhudiwa pia maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi huo, yaliyoonekana mjini Dodoma, Arusha na Mwanza. Waandamanaji wanadai uchaguzi ulikuwa na dosari. 

Hata hivyo muda mfupi baada ya maandamano kushuhudiwa, utawala nchini Tanzania ulichukua hatua za kudhibiti maandamano hayo ikiwa ni pamoja na kuwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi. Risasi za moto pia zinadaiwa kutumika katika juhudi za kuwadhibiti waandamanaji. Kulingana na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International, watu kadhaa wameuwawa na wengine kukamatwa tangu vurugu  hizi zilipoanza Oktoba 29. 

Serikali bado haijatoa maoni kuhusu idadi ya vifo lakini imesisitiza kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa amani na uwazi. 

Chama tawala nchini Tanzania  (CCM), ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru wake 1961, kinatarajiwa kuendelea kukita mizizi. Tayari matokeo ya awali yanamuonesha mgombea wake Samia Suluhu Hassan akiongoza kwa asilimia 94 ya kura dhidi ya wapinzani wake 16 anaochuana nao. 
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *