Wachambuzi wa Taasisi ya Rasilimali Duniani WRI, ambao hufuatilia uwasilishaji wa malengo hayo, wamesema zikiwa zimesalia siku chache kabla ya mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa wa COP 30 kuanza katika jiji la Belém, nchini Brazil, ni nchi 65 pekee ambazo tayari zimewasilisha rasmi malengo yao ya hali ya hewa. Hii inawakilisha takribani asilimia 36 ya utoaji wa hewa chafu duniani.
Utoaji wa gesi inayochafua mazingira unaotokana na uchomaji wa makaa ya mawe, gesi asilia na mafuta ndio unaosababisha mabadiliko katika hali ya hewa duniani na kuleta ukame, mafuriko, dhoruba na joto kali linaloua watu.
Imepita miaka 10 tangu kupitishwa kwa makubaliano ya kimataifa ya hali ya hewa ya mwaka 2015, makubaliano yenye malengo makubwa zaidi hadi sasa. Kulingana na makubaliano hayo, viongozi wa dunia waliahidi kupunguza ongezeko la wastani wa joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 2, na ikiwezekana kuzuia lisizidi nyuzijoto 1.5.
Nchi pia zilikubaliana kuhuisha na kuwasilisha upya malengo yao kila baada ya miaka mitano. Muda wa mwisho wa uwasilishaji ulikuwa mapema mwaka huu, na shinikizo sasa ni kubwa kwa mataifa kutangaza ahadi mpya za kuachana na matumizi ya nishati mbadala.
Simon Stiell, mkuu wa masuala ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, amesema kuwa kuna maendeleo halisi yanayopatikana, “lakini kasi yake inapaswa kuongezeka, na kuwa ya haki zaidi.”
Afisa wa Umoja wa Mataifa: Kasi na msaada kwa nchi masikini unahitajika
Katika taarifa iliyotolewa sambamba na ripoti ya Umoja wa Mataifa inayochambua malengo mapya ya hali ya hewa yaliyowasilishwa na nchi chini ya makubaliano ya Paris, Stiell amesema wanahitaji kasi zaidi, na msaada zaidi kwa nchi nyingi kuchukua hatua thabiti zaidi za hali ya hewa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, kama ahadi zilizotolewa zitatekelezwa, basi kutakuwa na upungufu wa takribani asilimia 10 ya utoaji wa hewa chafu duniani kufikia mwaka 2035.
Melanie Robinson, Mkurugenzi wa Mpango wa Hali ya Hewa, Uchumi na Fedha wa Kimataifa, WRI, amesema kuwa mabadiliko yanaendelea, akitaja uwekezaji katika nishati ya jua, magari ya umeme, na ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, ameongeza kuwa kasi ya utekelezaji bado ni ndogo mno.
Akizungumza na shirika la habari la The Guardian la Uingereza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kuwa dunia imeshindwa kuzuia kupanda kwa joto duniani kupita kiwango cha nyuzi joto 1.5 katika miaka michache ijayo.
Umoja wa Ulaya, China, na India ni miongoni mwa watoaji wakubwa wa hewa chafu ambao bado hawajawasilisha rasmi malengo yao.
Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa ya nia mwezi Septemba ikionyesha mpango wa kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kati ya asilimia 66.25 na 72.5 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990.
Hata hivyo, wadau wengine wanaonya kuwa mpango huo unaweza kuleta mkanganyiko, kupunguza imani ya wawekezaji na kudhoofisha ajira, usalama wa nishati na ushindani wa kiuchumi.
Wakosoaji wasema mchango wa nchini kubwa kama China bado ni mdogo
Wakati wa Wiki ya Hali ya Hewa ya New York mwezi Septemba, Rais wa China Xi Jinping pia alitangaza dhamira ya kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kati ya asilimia 7 hadi 10 kutoka kiwango chake cha juu, kiwango ambacho wachambuzi wanaamini China imekifikia au iko karibu kukifikia.
Wakosoaji wamesema ahadi hiyo ni ndogo mno, lakini wataalamu wameiambia DW kwamba China huenda ikatimiza na hata kuzidi lengo lake.
Watoaji wengine wakubwa kama Australia na Japan, ambao tayari wamewasilisha ahadi zao chini ya Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, wamekosolewa kwa ‘kukosa ujasiri wa kutosha na kutoonyesha uwiano wa haki katika jitihada zao.
Melanie Robinson amesema ingawa inatarajiwa kwamba watumiaji wakubwa wa gesi inayochafua mazingira kama China na Umoja wa Ulaya watawasilisha rasmi malengo yao kabla au wakati wa mkutano wa COP 30, bado kuna pengo kubwa.
Anasema nchi zinapaswa kuthibitisha upya lengo la nyuzi joto 1.5, kuharakisha mikakati maalum ya sekta kwa ajili ya kupunguza utoaji wa gesi chafu, na kufafanua njia za kufikia malengo hayo.
Ingawa mara nyingi vyombo vya habari huzingatia ahadi za kupunguza utoaji wa gesi chafu, nchi pia hujumuisha malengo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa msaada wa kifedha kwa mataifa yanayoendelea.