Katika kipindi kifupi tu cha uchaguzi ambapo machafuko yalitokea katika nchi hiyo, mataifa kadhaa jirani yaliathirika kiuchumi. Hii ni baada ya mtiririko wa bidhaa muhimu kama vile mafuta na pia huduma za mawasiliano kutatizwa.
Kusitishwa kwa muda shughuli kwenye bandari ya Dar es Salaam kuliathiri uchukuzi wa bidhaa muhimu zinazoagizwa na zile zinazouzwa katika mataifa ya kigeni hasa kutoka nchi za jumuiya ya kibiashara ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Kwa mfano, shughuli za forodhani zilisimamishwa kwenye mipaka ya Songwe na Kasumulu kati ya Malawi na Tanzania wakati waandamanaji walipokabiliana na polisi kipindi cha uchaguzi.
Makundi yalishambulia majengo ya serikali ya Tanzania, wakaharibu vitu katika ofisi za forodha na pia kuharibu vifaa vya mawasiliano Songwe.
Kulingana na Shirikisho la wachukuzi wa Malawi, hali hii imeathiri sana sekta ya usafirishaji shehena za bidhaa. Bwana mmoja kwa jina Sydney Chaima aliiambia DW kwamba hakuna mafuta kwenye vituo vya mafuta mjini Lilongwe,Malawi.
Hali kama hii ndiyo inaelezewa na wataalamu wa kiuchumi na kisiasa kwamba ukosefu wa uthabiti wa kisiasa una athari kubwa kwa uchumi wa mataifa jirani.
Akiongea na DW, msomi wa kiuchumi Christopher Mbukwa ametoa angalizo kuwa wanatarajia kupanda kwa mfumko ikilinganishwa na ukuaji wa kiuchumi. Wakulima ndiyo wataathirika zaidi katika kipindi hiki ambapo mbolea inahitajika.
Mataifa yanavyotegemea rasilimali za Tanzania
Mataifa ya bara ya Malawi, Zambia na Zimbabwe hutegemea pakubwa bandari za Tanzania kwa bidhaa za mafuta, dawa, pembejeo la kilimo, magari na nguo.
Tanzania ni moja kati ya mataifa wanachama wa jumuiya ya kiuchumi kusini mwa Afrika SADC na njia kuu za biashara kati ya mataifa hayo na nchi zingine za kaskazini hupitia nchi hiyo. Miundombinu hii inajumuisha barabara, reli na majini.
Asilia 60 ya biashara za SADC hupitia njia hizo. Mapema mwaka huu, mataifa wanachama wa SADC ikiwemo Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Zimbabwe zilipitisha mpango wa kujenga miundombinu inayobashiriwa kuleta mapato ya zaidi ya dola bilioni 16.1 za Kimarekani na kubuni fursa milioni 1.6 za kazi.
Takribani magari 15,000 yanayoagizwa Zimbabwe kutoka nje hupitia bandari za Tanzania kila mwaka.
Kulingana na mfanyabiashara Trice Chisamba ambaye anashiriki biashara ya magari Zimbabwe alifahamisha DW kuwa walishindwa kuwasiliana na mawakala wao wa forodhani kuendesha mchakato wa forodhani kutoka na kukatizwa kwa mitandao ya mawasiliano.
Hofu yake nyingine ilikuwa kwamba magari yao mengine yalikuwa yameruhusiwa kuondoka bandarini na zingaharibiwa katika ghasia.
Wadadisi wana mtazamo kuwa pana haja ya kuzingatia kutumia bandari za mataifa mengine kama vile Msumbiji au Afrika Kusini. Hata hivyo njia hizo zitakuwa za gharama za juu.
SADC wakosoa mazingira ya uchaguzi
Kwa upande wao, waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania kutoka nchi za jumuiya ya SADC walikosoa mazingira ya uchaguzi huo wakisema kuwa haukuafiki viwango vya demokrasia.
Sababu walizotoa ni kwamba wapigaji kura hawakupewa nafasi kufanya chaguo waliopendelea kutokana na hali ya kukandamiza shughuli za upinzani.
Ni kwa msingi huu ndipo wamemtaka rais Samia Suluhu kufanya juhudi kujenga mazingira ya amani na maridhiano mapya miongoni mwa Watanzania.
Kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais Suluhu, ni marais wawili tu kutoka SADC waliohudhuria. Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na rais wa Msumbiji Daniel Chapo.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa alimtuma makamu wake Constantino Chiwenga. Akizungumza kwenye televisheni ya Zimbabwe, Chikwenga alitaja Tanzania kuwa nchi ilikomaa kidemokrasia na inatambulika kuhusika katika juhudi za ukombozi na kwa hiyo ina uwezo kurekebisha hali na kusonga mbele.
Serikali ya Afrika Kusini haijatoa tamko lolote kuhusu hali ya Tanzania. Rais wake Cyril Ramaphosa alichaguliwa hivi majuzi kuwa kaimu mwenyekiti wa SADC. Hii ilikuwa baada ya mwenyekiti wa mwaka 2025 Andry Rajoelina kupinduliwa.
