Akizungumza Jumatano katika ujumbe wa video mjini Kiev Zelensky alisema mifumo ya ulinzi wa anga na ulinzi wa mifumo ya nishati ni “vipaumbele muhimu zaidi kwa kuzingatia mashambulizi ya Urusi. Alisema “Kwa kweli, wasambazaji wetu wa nishati, timu za ukarabati na vikosi vya ulinzi wa raia wana shughuli nyingi kila siku kurejesha eneo hilo baada ya mashambulizi.

Kuna mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya mstari wa mbele wa vita ya Chernihiv, Sumy,
Kharkiv, Donetsk, Zaporizhzhya, Kherson na Mykolaiv. Zelesnky alisema msaada wa kimataifa unapaswa kupangwa haraka iwezekanavyo huku mamlaka za mitaa za Ukraine zikiendelea kuchukua hatua.

Vita vinapoingia katika majira ya baridi ya nne, jeshi la Urusi kwa mara nyingine linavishambulia vituo vya umeme na vituo vidogo kwa utaratibu ili kuharibu usambazaji wa umeme, joto na maji kwa idadi ya watu wa Ukraine.

Kulingana na kampuni ya huduma za umeme ya Ukrenergo, mgao wa umeme unapangwa tena kote nchini Alhamisi ili kuleta utulivu kwenye mtandao. 

Ukraine imekuwa ikijilinda dhidi ya uvamizi kamili wa Urusi kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.

Kremlin: Ukraine inaficha hali mbaya upande wa mashariki

Jana Jumatano Urusi iliishutumu Ukraine kwa kuficha taarifa za kuzingirwa kwa wanajeshi wake katika miji ya mashariki ya Pokrovsk na Myrnohrad. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliyaambia mashirika ya habari ya Urusi kwamba Ukraine ilikataa pendekezo la Urusi la kuwaruhusu waandishi wa habari wa nchi za Magharibi kulitembelea eneo hilo, licha ya kutaka sana kwenda huko. Peskov aliuliza, “Ni nini kinachofichwa Kiev? Hali mbaya ya vikosi vyao inafichwa.” 

Mji wa Pokrovsk umekuwa kama nembo ya upinzani wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi
Mji wa Pokrovsk umekuwa kama nembo ya upinzani wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa UrusiPicha: Anatolii Stepanov/REUTERS

Jeshi la Ukraine limekataa mara kwa mara madai ya Urusi ya kuzingirwa katika eneo hilo.

Shirika la kijasusi la jeshi la Ukraine HUR hapo awali iliripoti operesheni za vikosi vyake maalum zinazolenga kuzuia kuanguka kwa mji wa Pokrovsk, jiji la madini ambalo hapo awali lilikuwa na wakazi wapatao 60,000 na limekuwa likipingwa vikali kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mji huo muhimu kimkakati unaonekana kama ishara ya upinzani wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Umuhimu wa jiji umeongeza uchunguzi wa maamuzi ya kijeshi ya Kiev. Zelensky amekabiliwa na ukosoaji wa hapo awali kwa madai ya kuchelewesha kujiondoa kutoka miji iliyopotea hapo awali, kama vile Bakhmut na
Avdiivka, kwa sababu za kisiasa.

Mnamo Septemba, Zelensky alimhakikishia Rais wa Marekani Donald Trump kwamba hali ya mstari wa mbele wa mapambano ya kivita imebaki imara.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewahimiza viongozi wa mjini Kiev kufanya maamuzi kwa maslahi ya raia na wanajeshi, akimaanisha mazingira huko Pokrovsk na Kupiansk katika eneo la Kharkiv.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema vikosi vyake huko Pokrovsk vingeendelea “kuviangamiza vitengo vya kijeshi vya Ukraine vilivyozingirwa,” huku vikizuia mashambulizi kutoka kwa Ukraine. Vikosi vya Urusi pia viliripotiwa kupanua udhibiti huko Myrnohrad, na kuimarisha zaidi kuzingirwa kwa wanajeshi wa Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *