Miami, Marekani. Shirikisho la Mpira wa Miguu la kimataifa (FIFA) limetangaza kuanzisha Tuzo ya Amani ya FIFA (FIFA Peace Prize), ambayo itatolewa kwa mara ya kwanza wakati wa droo ya Kombe la Dunia Desemba 5, 2025 huko Washington.
Kwa mujibu wa FIFA, tuzo hiyo itatambua matendo ya kipekee ya kuleta amani. Hata hivyo, rais wa FIFA Gianni Infantino, ambaye ana uhusiano wa karibu na Rais wa Merekani, Donald Trump, alikataa kufichua kama kiongozi huyo ndiye atakayekuwa mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo.
“Desemba 5 mtajua,” amesema Infantino alipokuwa akizungumza kwenye America Business Forum mjini Miami, muda mfupi baada ya Trump kuhutubia mkutano huohuo.
Mapema siku hiyo, Infantino amenukuliwa akisema: “Katika dunia inayozidi kuwa na migawanyiko na machafuko, ni muhimu kutambua mchango wa wale wanaofanya kazi kwa bidii kumaliza migogoro na kuwaleta watu pamoja kwa roho ya amani.”
FIFA imesema tuzo hiyo, ambayo mwaka huu itatolewa na Infantino mwenyewe, itakuwa ya kila mwaka, ikitolewa kwa niaba ya mashabiki wa soka kote ulimwenguni.
Trump alipitwa mwezi uliopita katika Tuzo ya Amani ya Nobel, licha ya jitihada za kumfanyia kampeni kutoka kwa viongozi wa chama chake cha Republican, baadhi ya viongozi wa dunia, na hata yeye binafsi.
Infantino, katika hotuba yake Jumatano, hakuficha ukaribu wake na Trump aliposema: “Nina bahati kubwa. Nina uhusiano mzuri sana na Rais Trump, ambaye namchukulia kama rafiki wa karibu.
“Bila shaka, amekuwa msaada mkubwa sana katika maandalizi ya Kombe la Dunia… Ana nguvu ya kipekee, jambo ambalo nalipenda sana. Anafanya mambo, anasema kile anachofikiria, na kwa kweli anasema yale watu wengi wanayofikiria lakini wanaogopa kusema. Ndiyo maana amefanikiwa sana.”
FIFA pia imeongeza uhusiano mwingine na familia ya Trump kwa kumteua Ivanka Trump, binti yake, kuwa mjumbe wa bodi ya mradi wa elimu wa dola milioni 100 unaofadhiliwa kwa sehemu na mapato ya tiketi za Kombe la Dunia 2026.
Infantino amesema tukio la droo ya Kombe la Dunia, ambalo litajumuisha pia utoaji wa tuzo hiyo ya amani, linatarajiwa kutazamwa na takribani watu bilioni moja duniani kote.