Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Iran iko tayari kusaidia juhudu za kutatua mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan ambao umeongezeka hivi karibuni kufuatia mapigano makali ya mpakani.
Araqchi amesema hayo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Pakistan, Mohammad Ishaq Dar, ambapo walijadili uhusiano wa pande mbili na matukio ya hivi karibuni ya kikanda na kimataifa.
Araqchi ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya sasa kati ya Afghanistan na Pakistan, akisisitiza haja ya mazungumzo endelevu kati ya pande hizo mbili, kwa msaada wa nchi zenye ushawishi mkubwa za kikanda, ili kutatua mizozo uliopo na kupunguza mvutano.
Pia ametangaza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu kutoa msaada wa aina yoyote kwa lengo kutatua mzozo huo.
Mwezi uliopita, majeshi ya Pakistan na Afghanistan yalipigana na kusababisha mauaji ya makumi ya watu, katika mvutano uliotajwa kuwa mbaya zaidi tangu Taliban waliposhika madaraka nchini Afghanistan, mwaka wa 2021.

Nchi hizo mbili jirani zilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano huko Doha mnamo Oktoba 19 wakati wa duru ya kwanza ya mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Qatar na Uturuki.
Pande hizo mbili zilianza duru nyingine ya mazungumzo ya amani mjini Istanbul siku ya Alhamisi iliyopita, lakini mazungumzi hayo yalivunjika siku iliyofuata.