Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema dunia haiwezi kulipa kisogo bara la Afrikam akisisitiza kuwa bara hilo ni nyumbani kwa karibu robo ya watu wote duniani, na lina nafasi kubwa ya maendeleo.

“Dunia haipaswi kuiacha Afrika. Ni mdau mkubwa sana, na uwezo wake ni mkubwa mno,” ameeleza Guterres alipozungumza na waandishi wa habari jijini New York baada ya Mkutano wa Tisa wa kila mwaka kati ya Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU), akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Mahamoud Ali Youssouf.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Afrika ina historia ndefu kama binadamu mwenyewe, na ina rasilimali nyingi ambazo zimechangia ukuaji wa uchumi wa mataifa mengi, lakini maendeleo yake yanakwamishwa na mfumo wa kifedha wa kimataifa ambao ni wa zamani na usio wa haki.

“Wakati umefika wa kurekebisha mfumo huu wa kifedha ili uakisi hali halisi ya dunia ya sasa na kuhudumia vyema mahitaji ya nchi zinazoendelea, hususan barani Afrika,” amesisitiza Guterres.

Ameongeza kuwa mageuzi hayo yanapaswa kuifanya mifumo ya kifedha kuwa jumuishi zaidi, yenye uwakilishi sawa, haki na ufanisi, kwa kutoa nafasi kubwa kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika taasisi za kifedha za kimataifa, kuongeza uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo, na kupunguza mizigo ya madeni kwa kutumia mbinu mpya za kifedha.

Kuhusu hali ya Sudan, Katibu Mkuu wa UN amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki mjini El Fasher, pamoja na kuongezeka mapigano katika maeneo ya Kordofan.

Guterres amegusia pia hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akisema miongo ya vita imezalisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambapo watu milioni 5.7 wamekimbia makazi na wengine milioni 21 wanahitaji msaada wa dharura.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf, amesema AU ina dhamira ya kufanya kazi na wadau wote wa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha mageuzi ya Baraza la Usalama la UN yenye uwazi, usawa na haki.

“Mageuzi haya ni muhimu sana na yataimarisha zaidi mfumo wa kimataifa wa ushirikiano,” amesema Youssouf…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *