
Mwakilishi wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina hapa mjini Tehran amesema: “sisi katika mavuguvugu ya Muqawama wa Kiislamu hatutambui uwepo wa utawala wa Kizayuni na hatulazimiki kuutambua, hasa kwa vile utawala huu hautambui hata uwepo wa watu wa Palestina.”
Nasser Abu Sharif, ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Televisheni ya Al-Alam na kusisitiza: “suala la Palestina si la kibinadamu tu, bali pia ni la kisiasa, na Wapalestina wanakabiliwa na uvamizi, kuzingirwa, na hatari ya kugawanyika.”
Mwakilishi wa Harakati ya Jihadul-Islamu hapa mjini Tehran amesema: “uhuru wa Palestina ni haki yetu ya asili, halali na ya kihistoria. Mashababi wa Muqawama ni watoto wa watu wa Palestina na wana haki ya utu, uhuru na kujitawala.”
Abu Sharif, ameendelea kueleza: “tangazo la Uhuru wa Palestina la mwaka 1988 na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanasisitizia haki halali na ya kisheria ya watu wa Palestina ya kujitawala na kujiamulia mustakabali wao”.
Amesisitiza kwa kusema: “Palestina yote, kuanzia baharini hadi kwenye mto wake, ni milki ya watu wake, na wazayuni wachokozi na wavamizi walikuja katika nchi hii kwa msaada wa miradi mikubwa ya kikoloni, kupitia mataifa makubwa ya wakati huo, Uingereza na Ufaransa, na baadaye chini ya usaidizi wa Marekani na hata Shirikisho la Kisovieti wakati huo”.
Mwakilishi wa Harakati ya Jihadul-Islamu hapa mjini Tehran ameeleza bayana kwamba, “hakuwezi kuwepo na amani ya kweli bila kupatikana haki za watu wa Palestina. Hatuwezi kuzungumzia kinachoitwa amani wakati Wapalestina wanakaliwa kwa mabavu na kumwagwa damu zao kila siku katika Ukanda wa Geaza”…/