Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kundi la waasi la M23 zimesaini makubaliano ya muundo kwa ajili ya mkataba wa amani unaolenga kumaliza mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana Jumamosi na wawakilishi wa pande zote mbili katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Qatar, pamoja na Marekani na Umoja wa Afrika, imekuwa ikishiriki mazungumzo ya mfululizo kwa miezi kadhaa sasa ili kumaliza mzozo katika eneo la mashariki ya DRC lenye utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, ambako kundi la M23 limekuwa likiteka miji muhimu.

Katika hafla hiyo, mpatanishi mkuu wa Qatar, ambaye ni Waziri wa Nchi, Mohammed Al-Khulaifi, aliyaelezea makubaliano hayo kama “ya kihistoria”, na kuongeza kuwa wadau wa mazungumzo wataendelea kufanya juhudi kufanikisha amani katika ngazi ya mashinani.

Mji mkuu wa Qatar, Doha umekuwa mwenyeji wa duru kadhaa za mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serikali ya DRC na M23 tangu mwezi Aprili, lakini mazungumzo hayo yalihusu zaidi masharti ya awali na hatua za kujenga imani.

M23, ambalo ni moja ya makundi ya waasi yanayoaminika kuwa yanaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, mwezi Januari liliiteka Goma, mji mkubwa wa mashariki mwa Kongo, na kisha likasonga mbele katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Tangu lilipopata nguvu tena za kijeshi mwishoni mwa 2021, kundi la M23 limeyatwaa maeneo mengi mashariki mwa Kongo kwa msaada wa Rwanda, jambo ambalo limesababisha janga kubwa la kibinadamu linaoendelea kushadidi katika maeneo hayo.

Hata hivyo serikali ya Kigali imekuwa kila ikikanusha kulisaidia kijeshi kundi hilo la waasi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *