
Dodoma. Watumiaji wa mafuta ya petroli na mafuta ya taa wataendelea kushuhudia ahueni ya kupungua kwa bei wakati ambao wanunuzi wa dizeli wataongeza kiasi kidogo cha fedha ili kupata lita moja ya mafuta hayo.
Kupungua kwa bei za petroli na mafuta ya taa kunaakisiwa na kushuka kwa gharama za kuagiza mafuta katika bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 2.4 kwa petroli na 3.6 kwa mafuta ya taa.
Hata hivyo, kulikuwa na ongezeko la asilimia 3.5 la gharama za uagizaji dizeli inayopitia bandari ya Dar es Salaam huku bandari za Mtwara na Tanga zikiwa hazina mabadiliko yoyote.
Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura), inayotangaza bei kikomo za mafuta zinazoanza kutumika leo Jumatano Desemba 3, 2025 inaonyesha lita moja ya petroli imepungua kwa Sh2.38 kwa yale yanayopitia bandari ya Dar es Salaam wakati bandari ya Tanga imepungua kwa Sh2.26 na Sh 2.45 kwa Mtwara.
Taarifa ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi wake, Dk James Mwainyekule imeeleza sasa lita moja ya petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam itauzwa kwa Sh2,749 kutoka Sh2,752, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,779 kutoka Sh2,704 na mafuta ya taa yatanunuliwa kwa Sh 2,653 kutoka Sh2,774.
Kwa wakazi wa Tanga, watanunua lita moja ya petroli kwa Sh 2,811 kutoka Sh2,813, dizeli lita moja ikiongezeka bei kutoka Sh2,766 iliyokuwapo Novemba mwaka huu hadi Sh2,840.
Kwa upande wa mafuta ya taa, wakazi wa Tanga watanunua lita moja kwa Sh2,714 ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,774.
Kwa wakazi wa Mtwara bei ya petroli itakuwa Sh2,842 ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,844, dizeli ikiuzwa kwa Sh2,872 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2,797 iliyokuwa ikiuzwa Novemba mwaka huu, huku mafuta ya taa yakishuka hadi Sh2,745 kutoka Sh2,866.
“Bei za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta
yaliyosafishwa katika soko la nchi za Kiarabu. Katika bei kikomo kwa Desemba
2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 1.7 kwa petroli,
asilimia 4.8 kwa dizeli na asilimia 6.4 kwa mafuta ya taa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia kwa bei za Desemba 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni imeongezeka kwa asilimia 4.48 kwani gharama za uagizaji (Premiums) zinalipwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani.
“Ewura imeagiza wauzaji wa mafuta nchini kutoa stakabadhi za mauzo kwa wanunuzi zinazoonyesha jina la kituo na bei halisi ya mauzo, na vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, wafanyabiashara wameruhusiwa kuweka bei zao shindani kulingana na soko isipokuwa kutozidisha bei kikomo zilizowekwa.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.”
“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.