Mbeya. Katika kuhakikisha  wataalamu vishoka wanadhibitiwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Mhandisi , Zena Ahmed amesema Serikali iko mbioni kutoa usajili kwa Bodi ya Wanajiosayansi Tanzania(TGS).

Hatua hiyo imetajwa kuiwezesha kusimamia , kuwasajili na kuthibitisha  wataalamu ili kudhibiti watu wasio sahihi,vishoka ambao wanaweza kuleta madhara katika tafiti mbalimbali hususani za uchimbaji  wa visima vya maji.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Desemba  3,2025,Katibu Mkuu Kiongozi  wa Serikali  ya Mapinduzi  ya Zanzibar Mhandisi ,Zena Ahmed  wakati akifungua Mkutano  wa Mwaka wa TGS, uliofanyika mkoani hapa.

Mkutano huo umehusisha  wataalamu,wanajiosayansi 4,000, kutoka Wizara mbalimbali ,Taasisi za Serikali na Vyuo vikuu.

“Lengo ni kuiwezesha bodi kuthibitisha na kuchuja watu wasio stahili kufuatia kuwepo kwa watu wanao jifanya wataalam kumbe sio mwisho wa siku wakaleta shida,”amesema.

Katika hatua nyingine amesema Serikali inatambua mchango mkubwa waTGS, katika ugunduzi na uendelezaji wa migodi ya madini ya aina  mbalimbali  sambamba na upatikanaji  wa rasilimali  za maji ardhini ,ugunduzi wa mafuta ,gesi na utafutaji wa nishati ya joto ardhini.

“Tunapo zungumzia utajiri wa rasilimali asilia kwa sababu  tumeshuhudia namna sekta ya madini  na wanajiosayansi wakiwa miongoni mwa msingi wa kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa,”amesema.

Wakati huo huo amesema  mkutano huo wa mwaka wakajadili namna TGS, inavyoweza kuchangia kufanikisha Dira ya Maendeleo yaTaifa 2050,elimu kwa jamii kuhusiana na  ajenda ya matumizi ya nishati safi na teknolojia  za kisasa .

“Mkutano huu umekuja wakati  nchi imetoka kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo  Endelevu ya mwaka 2025 na kuanza utekelezaji  wa Dira ya mwaka 2050,sasa wataalamu  tujadili namna bora ya kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kugeukia nishati safi ili kufikia malengo ya Serikali na kuokoa maisha ya watanzania, “amesema. 

Pia,  amewataka kuisaidia Serikali kufanya tafiti za kina ardhini na kwenye miamba ili kubaini maeneo yanayo stahili  kujenga makazi ya watu,uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.

Kwa upande wake Rais wa Wanajiosayansi Tanzania (TGS), Prof Elisante Mshiu amesema mchango wao ni kuendeleza na kukuza migodi ya wachimbaji  nchini na upatikanaji  wa rasilimali za  nishati ya mafuta na gesi.

Amesema wanaendelea  kushirikiana na  jumuiya za kimataifa na kikanda  hususani Afrika,Kenya Uganda na nyingine nyingi lengo ni kunufaika na fursa mbalimbali. 

Amesema pamoja na mchango  wa ugunduzi  wa rasilimali mbalimbali kuna changamoto ya kuzifanyia kazi licha ya  kuanzishwa kwa bodi ya usajili ya wataalam katika nyanja mbalimbali. 

“Ingawa kupitia Kamati tumepiga hatua kubwa katika kufanikisha suala hilo ,lakini tunaendelea kulifanyia kazi hivyo ili kuonekana mchango wetu tunaomba mchakato  wa kusajili bodi ufikie mwisho ili kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa  Endelevu 2050,”amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Beno Malisa, Katibu Tawala Msaidizi, Viwanja, Biashara na Uwekezaji, Anna Mwambene amesema  ufike wakati wataalamu kufanya tafiti za kina za hali ya  udongo ili  kudhibiti madhara hususani  kwa wachimbaji  wa madini.

“Utafiti  wa kidiolojia ufanyike kwa tija kubwa kwenye maeneo ya miamba na  ardhi ili kusaidia wachimbaji  wadogo  kutokana tamaa  ili kuongeza wigo mpana katika sekta ya madini mkoani hapa,”amesema.

Amesema Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya pili kitaifa katika sekta ya  madini ya dhahabu , hivyo kupitia mkutano huo wa  wanajiosayansi uje na matokeo makubwa kufanya kupanda hadi  kushika nafasi ya kwanza.

Kauli za wachimbaji. 

Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu Kijiji cha Saza Mkoa wa Songwe,Christopher  Fredy amesema wanakabiliana na changamoto ya ukosefu wa vifaa maalum vya kufanya tafiti katika maeneo ya uzalishaji na kuomba Serikali ione namna ya kuwafikia. 

“Tumekuwa tukichimba kwa mazoea kwa kutumia vipimo visivyo na uwezo mkubwa jambo ambalo linachangia uharifu wa mazingira kwa kuvamia maeneo mengi zaidi bila kufanikiwa,”amesema .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *