
Duru za habari zimeripoti kwamba wanajeshi na walowezi wa Kizayuni wameendelea kuvamia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kuchoma moto nyumba za Wapalestina na kushambulia raia wasio na ulinzi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, vikosi vamizi vya Israel jana Ijumaa viliendelea kuvamia maeneo kadhaa ya ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, lakini vijana wanamapambano wa Kipalestina walisimama kukabiliana nao kishujaa.
Ripoti zinaonesha kwamba wanajeshi vamizi wa Israel wamevamia mji wa Beit Ammar na kisha kitongoji cha Ain Sara huko Al Khalil na kurusha mabomu ya sauti. Duru za ndani za Wapalestina zimeripoti kutokea mapigano kati ya vijana wa Palestina na wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni kwenye maeneo hayo.
Uvamizi wa wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umeripotiwa pia kwenye mji wa Beit Furik huko Nablus, uvamizi ambao umefanyika mara kadhaa huku wanajeshi makatili wa Israel wakichoma moto nyumba na maeneo ya kilimo ya Wapalestina bila ya kujali chochote. Ripoti zinaonesha kwamba baada ya wanajeshi wa Israel kufanya uvamizi na kushambulia makazi ya raia, walifunga barabara kuu na kuzuia harakati za wananchi wa Palestina.
Utawala wa Kizayuni umeanzisha wimbi kubwa jipya la uvamizi na mashambulizi dhidi ya maeneo ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi, hasa kaskazini mwa eneo hilo katika hali ambayo tangu katikati ya mwezi Januari mwaka huu, sambamba na makubaliano ya mwanzo ya kusitishwa mapigano Ghaza, wanajeshi wao wamekuwa wakiyavamia mara kwa mara maeneo ya Ukingo wa Magharibi na kuwateka nyara vijana wa Palestina na kuwapeleka kusikojulikana.