Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland ametangaza kuwa Baraza la NATO na Russia limevunjwa rasmi huku kukiwa na wasiwasi wa kuibuka mivutano ya kijeshi kati ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Pars Today, Radosław Sikorski Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, ametangaza kuwa Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) umeamua kuvunja baraza hilo. Baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO mjini Brussels hivi karibuni, Sikorski alieleza kuwa Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, ametangaza kwamba” “Baraza la NATO na Russia halipo tena na sheria ya kuanzisha baraza hilo haina nguvu tena.”
Mahusiano kati ya Russia na NATO yalianza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mnamo mwaka 1997, pande zote mbili zilisaini sheria ya kuanzisha Baraza la NATO na Russia, kwa msingi kwamba hakuna upande utakaouchukulia upande wa pili kama adui, bali wataunda chombo cha mashauriano ya pamoja. Hatimaye, Baraza la NATO–Russia lilianzishwa rasmi mwaka 2002.
Hadi mwaka 2014, Russia na NATO zilishirikiana katika masuala kama vile kupambana na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya na uharamia baharini. Hata hivyo, kufuatia vita vya Ukraine, NATO ilisitisha ushirikiano wake na Russia. Mazungumzo kati ya pande hizo katika mfumo wa Baraza la NATO–Russia yalikoma mwaka 2019, na mnamo mwaka 2021 Russia ilisitisha shughuli za ofisi yake ya uwakilishi wa kudumu katika NATO mjini Brussels na kufunga ofisi za NATO mjini Moscow.
Mwelekeo wa mvutano unaoongezeka kati ya Russia na NATO unapata maana kwa kuzingatia hatua za kijeshi na kisiasa za muungano huu wa kijeshi wa nchi za Magharibi dhidi ya Moscow. Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti na kuvunjwa kwa Mkataba wa Warsaw, NATO ilijipatia tafsiri mpya ya majukumu na mipaka yake ya kijiografia, na ikaanza sera ya kupanuka kuelekea mashariki katika eneo la nchi zinazopakana na Russia. Mchakato wa upanuzi ulianza mwaka 1995 na kukamilika katika miaka ya 1999 na 2004 kwa kujiunga kwa nchi nyingi za Ulaya Mashariki na eneo la Baltiki. Macedonia Kaskazini ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na NATO.
Aidha, NATO imefanya juhudi kubwa za kuingiza kama vile Georgia na Ukraine, katika muungano huo wa kijeshi. Hatua hii, kwa mtazamo wa Russia ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa taifa. Hatimaye, hali hii ilisababisha vita vya Russia na Georgia mwaka 2008 na vita vya Russia na Ukraine vilivyoanza mwaka 2022 na vinaendelea hadi sasa.
Rais wa Russia, Vladimir Putin, ameeleza kuwa chanzo cha vita vya Ukraine ni upande wa Magharibi, ambao daima umekuwa ukijaribu kuisukuma Ukraine kujiunga na NATO bila kuzingatia wasiwasi wa kiusalama wa Moscow.
Katika mvutano wa maneno wa hivi karibuni kati ya Russia na NATO, Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia, alisema kuwa Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) ni adui wa nchi yake na akatoa onyo kwamba “adui akikataa kujisalimisha, ataharibiwa.”
Rais wa Russia, Vladimir Putin, jioni ya Jumanne alisisitiza kuwa nchi yake haina nia ya kuanzisha vita na Ulaya. Aliongeza: “Hatutaki kupigana na Ulaya, hili nimesema mara mia. Lakini iwapo Ulaya ghafla itaamua kuanzisha vita, basi tuko tayari kwa hali hiyo kuanzia sasa.”

Onyo kali la viongozi wakuu wa Russia kwa nchi za Ulaya limekabiliwa na majibu makali kutoka NATO. Katika muktadha huu, afisa mwandamizi wa NATO – ambaye jina lake halikufichuliwa – amedai kuwa jeshi la Russia huenda halina uwezo wa kukabiliana kijeshi na nchi za Ulaya. Afisa huyo alisema: “Putin anajua kwamba NATO, katika suala la kulinda washirika wake, imeungana zaidi kuliko wakati wowote ule.”
Aidha, aliongeza: “Muungano hautakaa kimya iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya ardhi ya mwanachama wake yeyote, na Russia haina uwezo wa kukabiliana na NATO kwa jumla.”
NATO, katika kukabiliana na vita vya Ukraine na kwa madai ya tishio la kimsingi kwa nchi za Ulaya wanachama wake kutoka Russia, tangu mwaka 2014 imeongeza uwepo wake wa kijeshi karibu na mipaka ya Russia na kupanua mazoezi yake ya kijeshi. Aidha NATO imeimarisha uwepo wake wa kijeshi katika upande wa mashariki wa muungano na kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine.
Kuongezeka kwa vita vya maneno kati ya Russia na NATO sambamba na kuvunjwa kwa Baraza la NATO–Russia sasa kunaweza kuchukuliwa kama hatua ya kihistoria katika uhusiano wenye mvutano kati ya pande hizo mbili. Baraza hili, lililoanzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuunda chombo cha mazungumzo, kujenga imani na kushirikiana katika masuala ya usalama. Hata hivyo halikuweza kutimiza matarajio ya awali. Tofauti za kimsingi kuhusu upanuzi wa NATO kuelekea mashariki, pamoja na migogoro ya Ukraine na Georgia, taratibu zililinyima baraza hili ufanisi wake halisi.
Sasa, kwa kuvunjwa rasmi kwake, swali kuu linalojitokeza ni: je, dunia imeingia katika hatua mpya ya mvutano kati ya Russia na nchi za Magharibi?
Kwa upande mmoja, hatua hii ni ishara ya kuporomoka kwa njia ya mwisho rasmi ya mazungumzo kati ya pande mbili. Katika hali ambayo vita vya Ukraine bado vinaendelea na NATO ikiimarisha uwepo wake wa kijeshi katika Ulaya ya Mashariki kwa kiwango kisicho na kifani, kuondoa chombo cha mashauriano kama hiki kunaweza kuongeza hali ya kutokuelewana na kupunguza uwezo wa kuzuia migogoro. Kukosekana kwa mazungumzo ya kimuundo kunapandisha hatari ya makosa ya kijeshi na kuongeza uwezekano wa makabiliano ya moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, Russia kwa kusisitiza uhuru wa kimkakati na ukaribu wake zaidi na China pamoja na nguvu nyingine zisizo za Magharibi, imeonyesha wazi kuwa haina hamu kubwa ya kudumisha mifumo ya pamoja na NATO.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba kuvunjwa kwa Baraza la NATO–Russia si mwanzo wa hali mpya kabisa, bali ni uthibitisho wa mchakato ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi. Mahusiano kati ya Russia na Magharibi tangu mgogoro wa Ukraine mwaka 2014 kimsingi yaliingia katika hatua ya mvutano wa wazi, huku ushirikiano wa kiusalama ukiwa katika kiwango cha chini zaidi.. Katika miaka ya hivi karibuni, baraza hili lilikuwa na sura ya kimaonyesho zaidi kuliko ufanisi wa kweli. Kwa hivyo, kuvunjwa kwake kunaweza kuchukuliwa kuwa tangazo rasmi la kuweko mgawanyiko baina ya pande mbili.
Mabadiliko haya yanaonyesha kwamba mahusiano kati ya Russia na Magharibi si tu kwamba hayataboreka katika muda mfupi, bali yameingia katika mkondo wa mvutano wa muda mrefu. Huu ni mvutano ambao kuliko wakati wowote unahitaji usimamizi wa kiakili na wa busara ili kuzuia migogoro au vita vya moja kwa moja kati ya pande hizi mbili.