
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf amepuuzilia mbali madai ya kukaririwa kuhusu visiwa vitatu vya Iran katika taarifa ya mwisho ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC), akiyaonya mataifa jirani kutoijaribu azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kulinda mamlaka yake ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hii.
Akihutubia kikao cha wazi cha Bunge mapema leo Spika Qalibaf amekosoa vikali madai yaliyoelezwa katika taarifa ya karibuni ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuhusu visiwa vitatu vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu Musa.
Mohammad Baqer Qalibaf amesema kuwa madai hayo yasiyo na msingi na ya kipuuzi, ambayo mara nyingi yanaathiriwa na mataifa mengine, ni kinyume na kanuni za kuheshimu mamlaka ya kujitawala na udumishaji wa uhusiano mwema na majirani.
“Iran inatoa wito kwa nchi jirani kujiepusha kuijaribu azma ya taifa la Iran katika kulinda umoja wa ardhi yake na visiwa vyake katika Ghuba ya Uajemi, ambavyo bado ni sehemu muhimu ya Iran,” ametilia mkazo Spika wa Bunge la Iran.
Ameongeza kuwa, Iran imekuwa ikitaka kuwepo utulivu, kudumisha amani na kuheshimu misingi ya ujirani mwema, huku ikitarajia majirani zake pia watafuata mkondo huo.
Visiwa vitatu vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu Musa kihistoria vimekuwa sehemu ya Iran; jambo ambalo linathibitishwa na hati nyingi za kihistoria, kisheria, na kijiografia. Hata hivyo, Umoja wa Falme za Kiarabu umekariri madai yake kuhusu umiliki wa visiwa hivyo.