
Mabadiliko ni mambo yasiyoepukika katika maisha ya binadamu, tangu anapoanza akiwa katika tumbo la mama mpaka anapomaliza mkataba wa kuwepo duniani.
Kwa kawaida mabadiliko ambayo kila mtu hutarajia na kupenda yatokee ni yale yanayompeleka hatua moja mbele na sio kurudi nyuma.
Katika siku za karibuni, Zanzibar imeshuhudia mabadiliko mengi, miongoni mwayo ni kupanua nafasi ya sekta binafsi kushiriki katika kuleta maendeleo, ikiwa pamoja na uwekezaji.
Lakini mabadiliko katika baadhi ya maeneo yametoa sura ya kurudi nyuma kuwapatia wananchi maendeleo, hasa katika huduma muhimu za kijamii.
Miongoni mwa maeneo ambayo sekta binafsi imepewea mkono mrefu ni sekta za afya na maji.
Serikali imeamua kutoa uwakala kwa utoaji wa huduma katika hospitali za kisasa zilizojengwa karibuni na ugawaji wa maji safi na salama.
Lakini matokeo yake, huduma hizi sasa zimezorota na yapo malalamiko kwamba kilichotokea ni sawa na kukitoa chakula kutoka kwenye kikaango na kukiweka kwenye moto.
Katika hospitali za mikoa zinazopendeza kwa majengo, huduma hazipendezi.Watu wanalalamika na kuona hali ikuwa afadhali kabla ya taaasisi binafsi kukabidhiwa uendeshaji na utoaji huduma zisiokuwa na huruma.
Wagonjwa wanapata usumbufu wa kila aina, kama kupoteza muda mwingi kuwaona madaktari wanaosemekana kuonekana kutojali wagonjwa.
Kwa mfano unaweza kwenda hospitali ya Kinazini, jirani na Shule ya sekondari ya Lumumba, saa 1 asubuhi na ikafika saa 4 ukaambiwa usubiri madaktari ambao hufika baada ya saa tatu.
Kwa maana nyingine wagonjwa wanaoambiwa mstahamilivu hula mbivu, wanajikuta wanalishwa iliyooza. Ni mashaka yasiyoelezeka.
Kwenye huduma za maji mambo hayasemeki. Baadhi ya maeneo hivi sasa yamekosa maji kwa zaidi ya miezi miwili kwa sababu kampuni ya Afrika ya Kusini iliyokabidhiwa kutoa huduma hiyo inaonekana kushindwa kuifanya kazi hiyo.
Kwa mfano, eneo moja la Bububu kama ilivyo katika sehemu nyingi za mjini na nje ya mji zimekosa maji safi na salama kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Lakini ada za malipo ya huduma zipo palepale licha ya hata tone moja la maji kutopatikana. Huu naweza kusema ni wizi wa kutotumia nguvu.
Kwa miezi miwili nimefuatilia suala hili, lakini unapoulizia Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), unaambiwa hawana mamlaka juu ya suala hilo na kukutaka uonanane na wahusika wa kampuni ya Afrika Kusini ya Running Water (Maji Yanayotiririka) ambayo tangu kuanza kwake kazi maeneo mengi sasa hayatiririki maji.
Kwa kweli uamuzi wa kutoa uwakala wa kutoa huduma huduma muhimu kama za matibabu na ugawaji wa maji unafaa kufanyiwa tathmini mpya.
Lakini tujiulize, je, ulifanyika utafiti wa kutosha kabla ya kufanyika uamuzi huu na kama ulifanywa, nani aliamua kuziondoa huduma hizi muhimu mikononi mwa serikali?
Ningetarajaia masuala muhimu kama haya yanayoathiri afya na usalama wa wananchi, yangefanyiwa uamuzi na wawakilishi wa umma waliopo kwenye Baraza la Wawakilishi na sio kikundi cha watu wachache kwa niaba wa wananchi wa Zanzibar.
Hata Wawakilishi wangepaswa kupata ushauri na mawazo ya wananchi kabla ya kufanyika uamuzi huu umuhimu.
Mtindo wa watu wachache kuamua hatima ya watu wa Zanzibar sio mzuri na ni vyema ukafanyiwa mapitio maana shida za matibabu na maji ambazo watu wanapata hivi sasa zinafikirisha na kuhatarisha maisha yao.
Kwa sasa Zanzibar inayo mamlaka ya maji, lakini haina mamlaka ya eneo hili na ipo tu kutunza mafali na unapoulizia matataizo ya upatikanaji wa maji unaambiwa mamlaka ipo kwa jina tu, lakini haina mamlaka wala madaraka katika suala hilo.
Watu hawakatai mabadiliko, lakini sio yanayowarejesha nyuma, kama tunavyoona ya mabomba ya maji safi kusambazwa kila pembe ya Visiwani, lakini yapo kama pambo tu na sio kuwapatia watu huduma hii muhimu.
Kila siku ukisiliza au kuangalia vipindi vya radio au runinga vya Shirika la Utangazi Zanzibar (ZBC), mada kubwa ya malalamiko ni huduma mbovu za afya na maji na wahusika wanaonekana hawajali.
Kuteleza katika uamuzi ni mambo ya kawaida. Ni vizuri kwa viongozi wa serikali kuinuka na kuanza safari mpya kwani huu ubinafsishaji uliopewa jina la uwakala kwa matumaini ya kutoa huduma bora hauna tija na umezusha mtafaruku katika jamii.
Kubwa zaidi ni kwa Serikali kuachana na mwenendeo wa mtu mmoja au kikundi cha watu kufanya peke yao bila ya baraka za Baraza la Wawakilishi na ushauri wa wadau juu ya masuala muhimu kama matibabu na upatikanaji wa maji.
Maeneo haya ndio roho ya maisha ya nchi na haifai kufanya mtihani wa kuyaweka rehani.