
Dar es Salaam. Washtakiwa 16 wanaokabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wamefikisha siku 34 wakiwa rumande kutokana na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Pia, shtaka la uhaini linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa hali hiyo, washtakiwa hao wataendelea kubaki rumande hadi Desemba 22, 2025, ambapo shauri lao litatajwa na upande wa mashtaka siku hiyo wataeleza hali ya upelelezi umefikia hatua gani.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao ambao na wenzao wamefutiwa mashtaka na kuachiwa huru, walifikishwa mahakamani hapo Novemba 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini.
Hivyo, tangu siku hiyo hadi leo Jumatano Desemba 10, 2025 washtakiwa hao wamefikisha siku 34 wakiwa rumande gerezani kutoka na upelelezi haijakamilika.
Hata hivyo, leo, wakili wa Serikali, Titus Aron ameieleza Mahakama hiyo upelelezi wa kesi hizo bado unaendelea.
Aron ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki wakati kesi hizo mbili zilipotajwa.
Wakili Aron amedai kesi hizo mbili zimeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.
“Kutokana na hali hiyo, tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia uwapo upelelezi umekamilika au laa,” amedai Aron.
Baada ya upande wa mashtaka kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi Robert Makoye, Paul Kisabo na Catherine Michael wameomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kwenda hatua nyingine.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, amewaeleza washtakiwa hakimu Hassan Makube anayesikiliza kesi zote mbili amepata udhuru, hivyo kesi hizo zimeletwa kwake kwa ajili ya kutajwa.
Hivyo ameziahirisha kesi hizo hadi Desemba 22, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa kesi yao dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kesi ya kwanza ni kesi ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26387 ya mwaka 2025 yenye wanne ambao ni Daud Joshua ambaye ni mshtakiwa wa 67; Joshua Thobias mshtakiwa wa 69; Michael Mariwa shtakiwa wa 78 na Irene Mabeche mshtakiwa wa 92.
Awali, kesi hiyo ilikuwa na jumla ya washtaka 94, lakini Novemba 24, 2025 l Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa 90 na kubaki wanne ambao ndio hao wanaendelea na kesi.
Kesi ya pili ya uchunguzi wa awali namba 26540 ya mwaka 2025 yenye jumla ya washtakiwa 12 ambao ni Jovin Kaaya mshtakiwa wa 25; Nelson Abisai maarufu Chuga ambaye ni mshtakiwa wa 26; mshtakiwa wa 27, Suphian Massawe; mshtakiwa wa 28, Kombo Helbert; (29)Rajab Machonjo; (30)Baraka Mwita; (31)Amasha Juma; (65)Fredy Chacha maarufu kama Chank; (66)Peter Chobe; (67)Mohamed Madea maarufu kama Teacher; (68) Tumaini Moshi na mshtakiwa wa 69 ni Gasper Mmari.
Vilevile, kesi hiyo ya pili, ilikuwa ya jumla ya washtakiwa 95, lakini Novemba 24 na Desemba 3, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa 83 na kibaki w 12 ambao ndio hao wanaendelea na kesi.
Kesi hizo za uchunguzi wa awali(PI) washtakiwa wote walisomewa mashtaka mawili; kula njama za kutenda uhalifu wa uhaini na shtaka la uhaini.
Kesi ya msingi:
Washtakiwa kwa pamoja walidaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Shtaka la pili, washtakiwa wote walidaiwa kuwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeneza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Washtakiwa hao walidaiwa kuwa walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Sarikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.