
Marekani imeshadidisha ghadhabu za walimwengu baada ya kutwaa meli ya mafuta ya Venezuela katika kile kilichotajwa na serikali ya Caracas kuwa hatua inayoshabihiana na uvamizi wa kijeshi wa Israel ulio kinyume cha sheria. Caracas iimekemea hatua hiyo ikiitaja kuwa ni “uharamia wa kimataifa.”
Caracas imekemea hatua hiyo ikiitaja kuwa ni “uharamia wa kimataifa.”
Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumatano alijigamba kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wameiteka meli kubwa ya mafuta ya Skipper katika pwani ya Venezuela inayobeba takriban mapipa milioni 2 ya mafuta ghafi . Baada ya wanajeshi wa Marekani kutwaa meli hiyo ya mafuta ya Venezuela, Donald Trump alisema: “Nadhani tutachukua mafuta.”
Kitendo hicho cha uharamia kilichofanywa na wanajeshi wa Marekani kwa kutumia helikopta zilizoruka kutoka kwenye meli ya kijeshi ya nchi hiyo, USS Gerald Ford, kinaashiria kampeni ya miezi minne ya mashinikizo ya Washington dhidi ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela.
Caracas kwa upande wake imelaani uharamia wa Marekani dhidi ya meli yake ya mafuta na kukitaja kitendo hicho kuwa “jinai kubwa ya kimataifa”.
Serikali ya Venezuela imesema kuwa “lengo halisi ni mafuta, nishati na rasilimali zetu ambazo ni mali za wananchi wa Venezuela.
Taarifa ya serikali ya Venezuela imeongeza kuwa: Marekani inafuata mbinu za Israel zilizokosolewa kwa muda mrefu za kunyakua rasilimali na kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine kwa kutumia nguvu za kijeshi ili kutimiza malengo yake ya kisiasa; yote hayo kwa kisingizio cha operesheni za usalama.
Maafisa wa Marekani wamedai kuwa meli hiyo ambayo iliwekewa vikwazo tangu mwaka 2022 ilikuwa sehemu ya mtandao haramu wa mafuta unaounga mkono makundi ya wanamgambo wa kigeni.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Washington inapanua uwepo wake kijeshi katika eneo la Carribean ili kufikia hifadhi kubwa ya mafuta ya Venezuela, sawa kabisa na namna Israel inavyohalalisha mabavu na ukandamizaji wake katika maeneo inayoyakaliwa kwa mabavu.