Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani mpango mpya wa Wazayuni wa kujenga nyumba 764 katika Ukingo wa Magharibi, ikiitaja hatua hiyo kuwa ni  ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa na azimio za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hasa Azimio nambari 2334.

Katika taarifa yake OIC imelaani vikali uamuzi wa utawala ghasibuu wa Israel wa kujenga nyumba mpya 764 na tangazo lake la mpango wa kuanzisha makazi mapya 17 katika Ukingo wa Magharibi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikibainisha kuwa hatua hizo ni sehemu ya mipango ya upanuzi na unyakuzi wa ardhi za Palestina inayofanywa na Tel Aviv.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, sera ya makazi ya utawala wa Kizayuni wa wa Israel inachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita na ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa na azimio za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hasa Azimio nambari 2334.

OIC imeashiria pia maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo yanathibitisha waziwazi kinyume cha sheria kwa vitendo vya uvamizi.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutekeleza majukumu yake na kuchukua hatua za haraka kusitisha vitendo vyote na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, ardhi yao na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakikosolewa kutokana na himaya na uungaji mkono wao kwa utawala ghasibu wa Israel na hata wengi wanaamini kuwa, himaya hiyo ndiyo inayoupa kiburi utawala huo ghasibu cha kuendeleza uharibifu na jinai zake huko Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *