
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Khan, amesema serikali ya Uingereza ilitishia kuikatia mahakama hiyo ufadhili na kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda taasisi hiyo, endapo jopo la majaji lingeendelea na mpango wa kutoa waranti wa kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Kauli hizo, ambazo ziliripotiwa kwa upana Alhamisi, zilitokea katika hati ambayo Khan aliwasilisha akitetea uamuzi wake wa 2024 wa kufungua mashtaka dhidi ya Netanyahu.
Ingawa Khan hakumtaja afisa wa Uingereza aliyehusika, alisema tishio hilo lilitolewa kupitia simu tarehe 23 Aprili 2024, ambapo afisa huyo alidai kuwa kutoa waranti dhidi ya Netanyahu na aliyekuwa waziri wa mambo ya vita, Yoav Gallant, kungekuwa “kupitiliza.”
Ripoti za vyombo vya habari zimeashiria kuwa huenda aliyepiga simu alikuwa waziri wa mambo ya nje wa wakati huo, David Cameron.
Khan pia alisimulia shinikizo kutoka kwa maafisa wa Marekani katika kipindi hicho hicho.
Alisema aliambiwa na afisa mmoja wa Marekani mnamo Aprili 2024 kwamba kutoa waranti kungeleta “athari mbaya sana,” na kwamba tarehe 1 Mei 2024, Seneta Lindsey Graham alimwambia kuwa kutekeleza waranti hao kungeifanya harakati Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina, Hamas, “iwafyatulie risasi” mateka wa Israel waliokuwa bado ndani ya Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa hati hiyo, Khan alikataa wito wa kuchelewesha mchakato huo, akisema hakukuwa na dalili zozote kwamba utawala wa Israel ulikuwa na nia ya kushirikiana na ICC au kubadili mwenendo wake Gaza, ambako Tel Aviv ilianza operesheni ya vita vya mauaji ya kimbari tangu Oktoba 2023.
Khan pia alitoa maelezo ya mlolongo wa matukio kuhusu madai ya “unyanyasaji wa kingono” yaliyomkabili mapema mwaka huo.
Alisema aliyasikia kwa mara ya kwanza tarehe 2 Mei 2024, na tarehe 6 Mei akafahamishwa kuwa malalamiko rasmi yalikuwa yamewasilishwa kwa kitengo cha ukaguzi wa ndani cha ICC ikiwa ni mbinu ya kumshinikiza.
Wakati huohuo, amesisitiza kuwa maandalizi yake ya keshi dhidi ya Netanyahu na Gallant yalikuwa “ya kina” na yaliongozwa na tathmini ya kisheria isiyoegemea upande wowote.
Khan pia amebainisha kuwa alisisitiza binafsi kutumwa kwa majibu makali ya kurasa 22 kwa ombi la Tel Aviv la kutaka waranti hao kufutwa.
Aidha, alieleza kuwa aliunda jopo la wataalamu wa sheria za kimataifa kuchunguza iwapo mahakama ina mamlaka ya kisheria—jambo ambalo Tel Aviv imekuwa ikilipinga—na kutathmini iwapo kesi dhidi ya Netanyahu na Gallant zinapaswa kufuatiliwa.