Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo yake na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia kwamba: BRICS inaweza kuandaa mazingira ya kuwepo ushirikiano wa haki na wenye uwiano katika ngazi ya kimataifa.

Rais Masoud Pezeshkian aliyasema hayo jana Jumamosi Tehran katika mazungumza yake na Tagesse Chafo, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia na kusema: BRICS inaweza kuwasilisha kigezo kipya cha mawasiliano ili kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama.

Pezeshkian ameashiria uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ethiopia katika kundi la BRICS na akalitaja kundi hilo la pande nyingi kuwa jukwaa la thamani na la kimkakati la kukuza ushirikiano, kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisiasa, na kukabiliana na hatua za upande mmoja katika mfumo wa kimataifa.

Rais wa Iran pia amesema: BRICS inaweza kuwa kigezo kipya cha mawasiliano kwa msingi wa pande mbili kuheshimu mamlaka ya kitaifa, umoja wa ardhi, tamaduni na staarabu mbalimbali na kuandaa uwanja wa kushirikiana kwa uadilifu na kwa mlingano. 

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia na ujumbe aliofuatana katika kikao na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran mjini Tehran 

Kundi la BRICS, linalojumuisha mataifa yanayoibukia kiuchumi zikiwemo Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini, pamoja na Iran, ni ishara ya mabadiliko ya mlingano wa nguvu katika karne ya 21. Ushirikiano kati ya nchi zinazoibukia kiuchumi husaidia kupunguza udhibiti wa Marekani na Magharibi kwa ujumla. Moja ya malengo ya BRICS ni kuunda mifumo huru ya kifedha na kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola. Hii inaweza kufanya mfumo wa kifedha wa kimataifa kuwa na mlingano zaidi. 

Kundi la BRICS pia limeanzisha Benki ya Maendeleo (NDB) na mipango ya dharura ya akiba ya fedha za kigeni hatua inayodhihirisha azma kuu ya kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa dunia. Wakati huo huo BRICS ni jukwaa la ushirikiano wa kisayansi, kiuchumi na kisiasa kati ya nchi huru na ni kigezo kilicho tofauti na mfumo unaotegemea udhibiti wa Magharibi. 

Kwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwa kwake mwanachama katika kundi la BRIC ni fursa kwa ajili ya kuimarisha sera yake ya nje iliyojengeka katika misingi ya pande nyingi, kujitawala na kukabiliana na vikwazo. 

BRICS ni jukwaa la kambi kadhaa ambapo ndani yake nchi mbalimbali, hasa nchi zinazoendelea, zina nafasi yake. Moja ya vitisho vikubwa zaidi vinavyotishia haki na uadilifu duniani ni madola ya Magharibi yanayotumia vikwazo kama wenzo. Kundi la BRICS linaweza kupunguza mashinikizo hayo kwa kuanzishai mifumo huru ya kifedha na kibiashara.

BRICS inasisitiza kuheshimiwa kwa mamlaka za kitaifa, tamaduni na staarabu mbalimbali; na hii inaweza kuwasilisha muundo tofauti kabisa na utaratibu unategemea satwa ya nchi za Magharibi. Iran pia kwa kushirikiana na nchi zinazostawi katika kundi la BRICS inaweza kuwa na nafasi athirifu zaidi katika kuundika kwa mfumo mpya wa dunia. 

Sera za nje za Iran siku zote zinasisitiza kujitawala na kukabiliana na ubeberu wa madola makubwa duniani. Kuwa mwanachama katika kundi la BRICS kunaimarisha suala hili na kuiweka Iran pamoja na mataifa yanayoibukia. Iran pia inaweza kujiweka mbali na utegemezi wa Magharibi kwa kuwepo kwake katika kundi hilo na hivyo kujielekeza kwenye kushirikiana na mataifa yanayoibukia kiuchumi kama China, Russia, India na Brazil. 

Kwa Iran, kuwa mwanachama ndani ya BRICS si tu kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo na mashinikizo ya Marekani, bali ni fursa ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisiasa na mataifa yanayoibukia kiuchumi na kuwa na mchango chanya katika mfumo wa kimataifa. 

Ushirikiano wa nchi huru katika kundi la BRICS utabadilisha mlingano wa nguvu duniani, utaimarisha kambi kadhaa, kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi na sarafu ya dola na utazidisha nafasi ya nchi zinazoendelea katika uchukuaji maamuzi kimataifa. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *