DAR ES SALAAM: WIZARA ya Afya imetangaza rasmi mwelekeo mpya wa kimkakati wa kuharakisha ujenzi wa viwanda vya dawa na bidhaa za afya nchini, kwa lengo la kuimarisha usalama wa afya wa Taifa,kupunguza utegemezi wa uagizaji wa dawa.

Hatua hiyo inalenga kuiweka Tanzania kwenye ramani ya uzalishaji dawa barani Afrika na duniani.

Akizungumza Desemba 24, jijini Dar es Salaam katika kikao cha wazalishaji wa dawa na bidhaa za afya ,Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa amesema kuwa ujenzi wa viwanda vya dawa si mpango wa majaribio bali ni uamuzi wa kimkakati ulioamuliwa na Serikali.

“Ujenzi wa viwanda vya dawa nchini Tanzania si jaribio ni mwelekeo wa kimkakati uliokwishaamuliwa na Serikali,” amesema Waziri Mchengerwa.

Mchengerwa amesisitiza kuwa usalama wa afya wa taifa hauwezi kujengwa kwa kutegemea uagizaji wa dawa pekee, bali unahitaji uzalishaji wa ndani unaokidhi viwango vya kimataifa, hususan WHO-GMP.

“WHO-GMP si anasa wala cheti cha mapambo ni pasipoti ya kuingia sokoni kimataifa,kwaajili ya kuuza bidhaa za afya,changamoto ya Tanzania katika biashara ya kimataifa ya dawa si ukosefu wa soko, wataalamu au fursa, bali ni viwango.

Akinukuu takwimu za hivi karibuni, amesema kuwa mwaka 2023 Tanzania iliuza dawa nje ya nchi chini ya Dola milioni 1, ikilinganishwa na Kenya iliyouza zaidi ya Dola milioni 140.

“Hili si tatizo la soko ni tatizo la viwango. Uharakishaji wa Uwekezaji na Mfumo wa Green-Lane Serikali imeeleza kuwa tayari imeanzisha mfumo maalumu wa uharakishaji wa uwekezaji kupitia Green-Lane Approval System, unaotekelezwa chini ya Pharmaceutical Investment Acceleration Programme, pamoja na kuunda Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce (PIAT) yenye mamlaka ya kufanya maamuzi ya haraka na kuratibu uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya dawa.

Ameongeza: “Tumeondoa urasimu wa maamuzi ya mizunguko mirefu. Mwekezaji mwenye nia ya dhati atapata majibu ya haraka, ya wazi na yanayotabirika”.

Amesema serikali imetangaza kuwa Tangazo la Expression of Interest (EOI) kwa ajili ya uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya tayari limetolewa rasmi, likiwa na lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na
wa kimataifa, kuhamasisha ubia wa kimkakati, na kuharakisha kufikiwa kwa viwango vya kimataifa.

“Mwisho wa kuwasilisha maombi ya EOI umetajwa kuwa ni tarehe 2 Machi 2026. Natoa wito kwa wazalishaji wa ndani kuwekeza katika ubora, teknolojia na mifumo ya viwango, msaada wa Serikali utaelekezwa kwa viwanda vinavyokidhi au vinavyoonesha mpango wa wazi wa kufikia viwango vya kimataifa.

Amesema hatalinda uzalishaji kwa sababu ni wa ndani pekee, bali watalinda uzalishaji wenye ubora unaokidhi viwango vya dunia. Aidha, ametoa onyo kali dhidi ya jitihada zozote za kuhujumu au kuchelewesha kwa makusudi ajenda ya industrialization ya sekta ya dawa, akisisitiza kuwa hii ni agenda ya taifa, si ya kikundi fulani.

Kwa waingizaji wa dawa, waziri amesema mabadiliko haya si tishio bali ni fursa ya kuingia katika uzalishaji wa ndani kupitia ubia, uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji wa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *