SIKU chache baada ya Mwanaspoti kuripoti kuwa John Bocco atarejea Simba, nyota huyo tayari ametambulishwa na kuanza rasmi kazi ya kocha wa timu ya vijana wa timu hiyo, ikielezwa amewekwa huko ili kusaka uzoefu kabla ya kuja kupewa jukumu katika timu ya wakubwa kama Seleman Matola.

Bocco aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu saba akitwaa nayo ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo kabla ya kutemwa misimu miwili iliyopita na kuibukia JKT Tanzania amerejeshwa Msimbazi akiwa kama kocha na amepewa kazi timu ya vijana ili kunoa ujuzi akipigiwa hesabu kubwa na klabu hiyo.

Kabla ya kuitumikia Simba, Bocco alikuwa Azam aliyopanda nayo Ligi Kuu tangu 2008 na kuituimikia kwa misimu tisa, akitwaa nayo taji la Ligi Kuu Bara 2013-2014, mataji matano ya Kombe la Mapinduzi na moja la Kombe la Kagame 2024, akishikilia pia rekodi na kufunga mabao 156 katika Ligi Kuu Bara kupitia misimu 16 akiwa ndiye kinara akimpiku Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyekuwa akiongoza kwa kufunga mabao 153 ndani ya misimu 13.

Awali, Mwanaspoti Desemba 19 liliripoti kuwa Bocco atarejea Simba akitokea JKT Tanzania aliyojiunga nayo baada ya kumaliza mkataba na Wekundu hao na kuifungia mabao mawili, kabla ya kudaiwa amejikita kwenye ishu na ukocha aliouanza tangu akiwa hapo Msimbazi.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba Bocco aliyeitumikia Simba kwa mafanikio inaelezwa licha ya kuachiwa timu ya vijana uongozi una mpango wa kumpandisha timu ya wakubwa mara baada ya kocha msaidizi wa timu hiyo, Suleiman Matola kumaliza mkataba kupelekwa kuongeza ujuzi nje ya Tanzania.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kimeliambia Mwanaspoti, Bocco kapelekwa timu ya vijana ili kuendelea kutafuta uzoefu, lakini mpango wa Simba ni kumsogeza timu ya wakubwa mara baada ya Matola kumaliza mkataba aliokuwa nayo tangu alipotua akitokea Polisi Tanzania mwaka 2019.

“Simba ina mpango wa kwenda kumsomesha Matola nje ya Tanzania kwa kozi ya miezi sita, hivyo kama hilo litatimia basi Bocco atapandishwa timu ya wakubwa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; “Matola hata akishindwa kwenda kozi ana mpango wa kuondoka Simba kutafuta changamoto nyingine kwenye timu ya Ligi Kuu Bara akiwa kocha mkuu, hata msimu huu kapata ofa nyingi lakini amegoma kuchukua timu katikati ya msimu.”

Chanzo hicho kimesema Matola alipata ofa kutoka KMC, lakini hajataka kutokana na kutaka kusimamia timu atakayoanza nayo mwanzoni mwa msimu na kuhusika kwenye mchakato wa usajili moja kwa moja ili lawama ikitokea aibebe yeye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *