Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Januari 13, 2026 kuanza kusikiliza ushahidi wa upande w Jamhuri katika kesi ya kuchepusha fedha na kuisababishia Wizara ya Tamisemi hasara ya Sh165 milioni, inayowakabili washtakiwa 13, wakiwemo wakuu wa idara wa manispaa ya Kigamboni.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba  21510 wa mwaka 2025 ni aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha na mhasibu wa Manispaa ya Kigamboni, Jonathan Manguli(38).

Wengine ni aliyekuwa mhasibu wa Manispaa hiyo Godfrey Martiny(44), aliyekuwa mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa mazingira wa Manispaa hiyo, Juvenalis Mauna(53),  Josephat Mutembei( 39) na aliyekuwa ofisa ugavi msaidizi wa Manispaa hiyo, Bibiana Mdete(53).

Pia yupo, aliyekuwa ofisa ugavi, Henry Rugayi(38),    Annie Maugo (43), ofisa hesabu kutoka Tamisemi Dodoma, Tumsifu Christopher(46) na ofisa hesabu, Aidan Mpozi(61) wote kutoka Manispaa ya Kigamboni.

Wengine ni wafanyabiashara Hamis Manfred(40), Paulo Mwakyusa(43), Godwin Cheyo(33) na Jennifer Manguli(30).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo, kutakatisha fedha na kuongoza genge na kufanya ubadhilifu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Desemba 29, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kupe a nyaraka za zitakazotumiwa na upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Hakimu Makube alisema upande wa Jamhuri utawapatia nyaraka hizo washtakiwa hao Januari 6, 2026 na kisha kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi Januari 13, 2026.

Awali, wakili wa Serikali Eric Davies aliileza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya washtakiwa kupewa nyaraka za maelezo ya mashahidi kabla ya kesi hiyo kuanza usikilizwaji.

Hata hivyo, wakili Davies aliieleza mahakama hiyo kuwa nyaraka hizo bado hazijakamilika kuchapwa hivyo aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya washtakiwa hao kupewa nyaraka hizo.

Davies baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Makube alimuelekeza awasiliane na mchapaji ili wajue nyaraka hizo zitakuwa tayari lini.

Davies alifanya hivyo na kesi hiyo iliahirishwa kwa muda ili awasiliane na mchapaji wa nyaraka hizo na baadaye kesi hiyo ilipoitwa tena mahakama, Jamhuri iliieleza mahakama kuwa bado hawajawakilisha na kwamba nyaraka hizo zitakuwa tayari Januari 6, 2026.

“Naelekeza Januari 6, 2026, saa nane mchana,  washtakiwa mtapewa nyaraka zenu na Januari 13, 2026 kesi itaanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri” alisema Hakimu Makube na kisha kuahirisha kesi hiyo.

Kati ya mashtaka hayo 10, matatu ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kupotosha mwajiri wao, mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu, mawili ni ya ubadhilifu wa fedha, moja ni kuchepusha fedha, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Tamisemi.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wanane ambao ni Manguli, Martiny, Mauna, Mutembei,Rugayi, Maugo na Kachira, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, wakiwa watumishi wa umma  kwa kuvunja sheria na kushindwa kutimiza majukumu yao walifanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh165 milioni.

Shtaka la pili ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili wafanyabiashara wanne ambao ni Manifred, Mwankyusa, Cheyo na Manguli ambao wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 ndani ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa sio watumishi wa umma na kwa kushirikiana na watumishi wa umma, kwa makusudi waliongoza genge ka uhalifu kwa kufanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh165 milioni.

Shtaka la tatu ni kuchepusha fedha linalowakabili  mshtakiwa Maugo, Kachira na Mpozi, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Septemba 5, 2023 katika ofisi za Tamisemi Dodoma, wakiwa wahasibu , kwa maslahi yao binafsi walichapisha na kuhamisha fedha kiasi cha Sh165 milioni, ambazo zilitakiwa zitumike kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Tamisemi.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa shtaka la nne ni ubadhilifu wa fedha linalomkabili mshtakiwa Manguli, Martiny na Mauna, ambapo wanadaiwa kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni wakiwa watumishi wa Manispaa hiyo, kwa nyadhifa zao za uhasibu, mkuu wa idara ya fedha na mkuu wa idara ya udhibiti taka na usafi wa mazingira, walibadilisha matumizi ya Sh128 milioni kwa masilahi yao  binafsi, fedha ambazo ziliwafikia mikononi mwao  kama wahasibu.

Pia, kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, wakiwa wahasibu walifanya ubadhilifu kwa kubadilisha fedha kiasi cha Sh36.8 milioni, fedha ambayo iliwafikia mikononi mwao kama wahasibu

Shtaka la sita ni matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumposha mwajiri wao ambaye ni Manispaa ya Kigamboni inayomkabili Manguli na Mutembei, ambapo wanadaiwa Februari 2, 2023 katika ofisi za Manispaa hiyo, kwa nafasi zao za  mhasibu na mhandisi na kwa nia ovu na kwa makusudi walimdanganya mwajiri wao kwa kutumia nyaraka iliyokuwa na taarifa zisizosahihi za taarifa ya ukaguzi wa vifaa, kuonyesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za moramu na kukodi greda kutoka kampuni ya Konya Investment Co Ltd, jambo ambalo walijua wanampotosha mwajiri wao.

Shtaka  la saba ni matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumposha mwajiri, linalomkabili Mdete, ambapo Februari 2, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, mshtakiwa akiwa Ofisa Ugavi Msaidizi, kwa nia ovu dhidi ya mwajiri wake, alitumia nyaraka

iliyokuwa na taarifa potofu ya vifaa kuonyesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za moramu na kukodi greda kutoka kampuni ya Konya Investment Co Ltd na kukodi greda, wakati wakijua kuwa wanampotosha mwajiri wao.

Vilevile, mshtakiwa Rugayi anadaiwa Machi 27, 2023 katika ofisi za Manispaa hiyo, mshtakiwa akiwa ofisa ugavi aliwasilisha nyaraka ya iliyokuwa na taarifa potofu ya vifaa, akionyesha kampuni ya Mbogholo Investment imepeleka tripu ya moramu kwenye  lori moja la futi 12 na kukodi greda, wakati akijua anampotosha mwajiri wake.

Shtaka la tisa ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa 12, isipokuwa mshtakiwa wa tano( Mdete) ambapo kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, washtakiwa walijihusisha na muamala wa fedha kiasi cha Sh165 milioni, wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la uchepushaji fedha.

Pia, washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho, kwa pamoja na huku wakifahamu na kwa nia ovu waliisababishia hasara Tamisemi ya Sh165 milioni.

Hata hivyo, mshtakiwa Mdete yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana na pia hana shtaka la kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Septemba 3, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 21510 wa mwaka 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *