
Nchini Guinea, ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma imetangaza siku ya Jumanne jioni, Januari 6, 2026, kifo cha Kanali Claude Pivi, aliyekuwa msaidizi na mshirika wa karibu wa Kapteni Moussa Dadis Camara, mkuu wa zamani wa utawala wa kijeshi uliotawala Guinea kati ya mwezi Desemba 2008 na Desemba 2009.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Conakry, Moktar Bah
Kanali Pivi alihukumiwa kifungo cha maisha kufuatia mauaji ya Septemba 28, 2009 katika uwanja wa Conakry, ambapo wafuasi wa upinzani walikuwa wamekusanyika kupinga uwezekano wa Kapteni Moussa Dadis Camara kugombea katika uchaguzi wa urais wa 2010.
Kanali Claude Pivi ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa kesi ya mauaji ya Septemba 28, 2009 huko Conakry, amefariki Jumanne, Januari 6, 2026, ofisi ya Mwanasheria Mkuu imetangaza.
Kanali Pivi alitoroka gerezani mara tu baada ya kuhukumiwa, wakati wa operesheni ya kundi la watu wenye silaha iliyowashangaza wengi mnamo Novemba 4, 2023, ambayo pia ilisababisha kutoroka kwa washtakiwa wengine kadhaa, akiwemo kiongozi wake wa zamani, Moussa Dadis Camara. Alikamatwa nchini Liberia na kisha kupelekwa Guinea mnamo Septemba 17, 2024, baada ya kuwa mafichoni kwa miezi kadhaa.
Matatizo ya kiafya yanayohusiana na kisukari
Mauaji ya Septemba 28, 2009 yalitokea wakati wa mkutano wa upinzani. Yalikandamizwa kwa nguvu na jeshi, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 156, mamia ya visa vya ubakaji, na mamia ya watu kujeruhiwa.
Tangu aliporudi, Kanali Pivi alikuwa akitumikia kifungo chake katika gereza lenye ulinzi mkali la Coyah, karibu na mji mkuu wa Guinea. Kulingana na mwendesha mashtaka katika Mahakama ya Rufaa ya Conakry, amefariki katika hospitali ya kijeshi ambapo alikuwa amekimbizwa kwa matibabu ya dharura kufuatia matatizo ya kisukari.