Dar es Salaam. Wakati meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ akiendelea kupambania afya yake kitandani, mke wake Sweet Fella, ametoa ufafanuzi kuhusu alichokiandika mtandaoni .
Sweet Fella amezungumza na Mwananchi na kusema, ameamua kuandika kuhusu Mkubwa Fella kutengwa na watu wake wa karibu kwa kushindwa kumjulia hali sababu kuna baadhi wanaamini anasaidiwa Diamond jambo ambalo siyo kweli.
“Mimi sijaandika kwenye akaunti yangu ya Instagram ili nipate kulipwa wema wa mume wangu kwa yale mazuri aliyowasaidia au kuwafanyia watu, hii hapana. Mimi nimetoa dukuduku langu watu wajue napambana mwenyewe ili mume wangu apone.
“Maana kipindi yuko mzima kuna simu kibao za watu walivyokuwa wananipigia usiku wa manane hadi Alfajiri nimuamshe mume wangu wana ishu naye. Yaani ilikuwa wakimkosa, mimi ndio nilikuwa napata shida walikuwa wananiambia nimuamshe mkubwa kuna ishu naye, sasahivi hizo simu sizioni tena,”amesema
Vipi kuhusu Diamond Platnumz kutoa sapoti?
“Kuhusu Diamond Platnumz, kutomsaidia Fella, yaani huwezi kumlazimisha mtu kwamba kwanini husaidii? Kwani yeye mwenyewe hajui kama Fella anaumwa? Si anajua bosi wake anaumwa.
“Hata kama ndio alitusaidia tukaenda India tukarudi, lakini asingeishia njiani na kukaa kimya. Sasa mimi kama nimetoa dukuduku langu sisaidiwi na mtu maana watu wanaweza kusema napata msaada kwa Diamind ambaye ni tajiri anamsaidia”.
Hali ya Fella ikoje kwa sasa?
“Hali ya mume wangu kwasasa hajambo, anaendelea vizuri na mazoezi. Maana kwa mwezi anatumia milioni moja na laki mbili kwa ajili ya mazoezi na toka ameanza kuumwa hadi sasa anatimiza mwaka mmoja.
“Mbali na hayo mazoezi kuna kwenda kliniki na kuna dawa za kununua kila wakati ili atumie. Ndio maana nasema napambana mwenyewe, hapa kuna familia inanitegemea yaani kila kitu kinaniangalia mimi, nazidi kumuomba Mungu ampe afya njema mume wangu arudi kama zamani”.
Awashukuru watu hawa Said Kessy , Muddy K na Mbosso
“Kiukweli kuna watu ambao sitaacha kuwashukuru ambao wamebakia na Mkubwa Fella hadi sasa. Na wanatoa sapoti kubwa sana kwake ni Mbosso na shemeji zangu Meneja Said Kessy, na Muddy K. Hawa wananisaidia sana na hata juzi wamemletea baiskeli ya kutembelea Mkubwa Fella, sababu bado hajaanza kuchanganya kutembea vizuri”.
Alichoandika kwenye Akaunti yake ya Instagram
Januari 4, 2026 Sweet Fella, ambaye mke wa Meneja wa wasanii maarufu Mkubwa Fella, ameshusha ujumbe mzito kupitia akaunti yake ya Instagram akielezea masikitiko yake juu ya mumewe anavyopuuzwa na watu aliowahi kuwasaidia, wakati huu akiwa anaumwa. Aliandika hivi :
“Mume wangu kuugua ni ibada mimi mke wako nipo pamoja na wewe mpaka dakika za mwisho ulipo mimi nipo. Leo hii hakuna mtu yeyote anayekuuliza hali lakini najua mambo yote uliyowafanyia na wanajua ila wanajizima data wote uliowasaidia”
“Pia wanaonisapoti nawatambua inshallah Mungu atawalipa kwa hicho mnachojitolea Mungu awasaidie. Namuombea Mume wangu apone atakuja kuongea mwenyewe yote.”
Mkubwa Fella ni miongoni mwa watu waliowahi kusimamia wasanii wakubwa nchini Tanzania na mchango wake kwenye muziki wa Bongo Fleva ni mkubwa. Mashabiki na wadau sasa wanahimizwa kumkumbuka katika sala na kumtakia nafuu.
Tujikumbushe Mkubwa Fella akizungumzia Afya yake na Mwananchi.
Machi ,4, 2025 Mwananchi iliripoti hali ya kiafya ya Mkubwa Fella aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Hata hivyo Fella alisema afya yake imezidi kuimarika baada ya kutoka India kupata matibabu, ambapo huko India gharama zote aligharamia Diamond Platnumz .
Ilipofika Mei, 2025 Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo. Alikata tamaa ya kupona lakini kwa wakati huo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.
“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.
“Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Mkubwa Fella.
Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii Januari , 2025 kuwa amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.
Hata hivyo baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu alikuwa anashindwa.