Ni siku 90 sasa tangu Humphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na Malawi, kuvamiwa na kutoweka wanafamilia yake wamekwenda katika nyumba aliyokuwa akiishi na kufanya sala maalum.
Kuanzia saa saba mchana, wanafamilia hao waliwasili katika nyumba hiyo, kisha wakafungua mlango na kuanza kukagua chumba baada ya chumba.
Simanzi na vilio vilitawala baada ya mama mzazi wa Polepole, Ana Maria polepole kuingia katika chumba alichokuwa akilala mtoto wake Humphrey, na kukuta damu iliyoganda ikiwa imesambaa ndani ya chumba. Mama yake Polepole, Ana Maria amesisitiza anachotaka ni mtoto wake kurudishwa akiwa hai.
“Hivi najua ya kwamba huko aliko si mzima hata kidogo, ni hilo tu watu wa Mungu, wamrudishe mwanangu akiwa mzima, lolote litakalotokea, na mimi nilizaliwa na Mungu kutoka mbinguni.”
Mara baada ya kukusanya baadhi ya mali za Polepole, wanafamilia hao walifanya sala maalum kumuombea ndugu yao, sala iliyoongozwa na kaka yake, Godfrey Polepole.
“Malaika ambao ni walinzi wetu tunawatuma, wakazungumze na wanaomshikilia ndugu yetu.”
Aghalabu wanafamilia hao wamesema kuwa pamoja na kukuta nyumba hiyo ikiwa imeharibiwa kwa kuvunjwa vitasa, kadhalika wamebaini kuwa kasha la kuhifadhi fedha, funguo za gari, kompyuta nane na simu, 5 vimechukuliwa.
Godfrey ameeleza kuwa, pamoja na kubaini uharibifu huo kadhalika funguo za gari na funguo za pikipiki za Humphrey zote zimechukuliwa akilituhumu jeshi la polisi kufanya hayo.
Wakili wa wanafamilia hao, William Maduhu amesema mpaka sasa ni miezi mitatu tangu Polepole atoweke na hivyo wanafamilia hao wanaitaka serikali na mamlaka husika ieleze alipo Polepole na iwapo ana makosa basi apelekwe mahakamani.
“Na nataka nirudie tena hapa kuitaka serikali ya Tanzania na mamlaka zote nchini, balozi polepole yupo wapi na huko aliko ana hali gani,kwa sababu nchi hii inaongozwa na sheria”
Humphrey Polepole, mwanaharakati, kada wa CCM, Balozi aliyewakilisha Tanzania kwa nyakati tofauti katika nchi za Cuba na Malawi, mjumbe wa bunge maalum la Katiba, alivamiwa na kisha kutoweka usiku wa kuamkia Oktoba 5 katika nyumba aliyokuwa akiishi, eneo la Ununio, jijini hapa na mpaka sasa hajulikani alipo.
