Abiria na watumiaji wa huduma za viwanja vya ndege Zanzibar wamehimizwa kutembelea Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar katika Kituo cha maonesho Dimani ili kutambua haki zao wanapokuwa safarini kwa usafiri wa anga.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume aliyeongeza kuwa abiria wanapokuwa katika viwanja vya ndege wanapaswa kufahamu masuala mbalimbali ya usafiri wa anga yakiwemo haki na wajibu.

“Tunalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya usalama wa anga, matumizi sahihi ya teknolojia ya ndege nyuki kwa mujibu wa sheria na kanuni, pamoja na haki za abiria, hatua inayochangia kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuimarisha usalama wa anga nchini.” Amesema Mohamed Ali Mohamed

Sambamba na hilo TCAA imewahimiza watumiaji wa ndege nyuki (Drone) kwa ajili ya shughuli mbalimbali visiwani Zanzibar wakiwemo waandaaji wa maudhui ya televisheni na mtandanao ikiwemo picha jongefu kusajiliwa na TCAA na kufuata miongozo ya mamlaka hiyo ya matumizi salama ya ndege nyuki.

Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yameanza tarehe 29 Desemba, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Januari, 2026.

Mhariri @moseskwindi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *