
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo jijini Geneva nchini Uswisi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) uchaguzi huo utafanyika huku kukiwa na mazingira ambamo raia wamenyimwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kujiunga na vyama kuelekea siku ya kupiga kura, tarehe 15 mwezi huu wa Januari.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ametoa wito kwa serikali ya Uganda kuheshimu haki za raia wote kushiriki katika masuala ya umma ya nchi yao bila uoga.
“Mamlaka za Uganda lazima zihakikishe kuwa waganda wote wanaweza kushiriki kikamilifu na kwa usalama katika uchaguzi, kama ilivyo haki yao chini ya sheria za kimataifa,”
Türk ameongeza kuwa. “Lazima wahakikishe kuwa hakuna nguvu isiyo ya lazima au iliyopitiliza, ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha za moto, inayotumiwa kutawanya maandamano ya amani.”
Mamlaka zatumia sheria kubinya uhuru
Ripoti hiyo inaeleza jinsi mamlaka zimetumia sheria zilizotungwa au kurekebishwa tangu uchaguzi uliopita wa mwaka 2021, ikiwemo Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta (Marekebisho) ya 2022, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Marekebisho) ya 2024 na Sheria ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (Marekebisho) ya 2025, kuwanyamazisha watu wenye maoni tofauti. Inabainisha kuwa viongozi wa upinzani wamekuwa wakikamatwa, ofisi za vyama kuvamiwa, na vyombo vya habari kudhibitiwa.
Vyama vya upinzani vimebinywa, viongozi wako korokoroni
Inatajwa kuwa chama cha National Unity Platform (NUP) kimekuwa kikikabiliwa na vizuizi vikubwa vikiwemo kuzuiliwa kwa mikutano yao na viongozi wao kuwekwa kizuizini ndani ya nyumba zao.
Wakati hayo yakijiri, Kiongozi mkuu wa upinzani Kizza Besigye anasalia kizuizini kwa mashtaka ya uhaini tangu aliposhikiliwa katika nchi jirani ya Kenya mnamo Novemba 2024. Yeye na mshirika wake Obeid Lutale wamenyimwa dhamana mara kwa mara.
Vilevile kukamatwa hivi majuzi kwa mtetezi mashuhuri wa haki za binadamu Sarah Bireete, pamoja na agizo la Serikali kuweka marufuku ya utangazaji wa moja kwa moja wa maandamano ya amani.
Risasi za moto zatumika kutawanya waandamanaji
Ofisi ya Haki za Binadamu imeelezea wasiwasi wake juu ya vikosi vya usalama, vikiwemo polisi, wanajeshi na Kikosi Kazi cha Pamoja cha Kupambana na Ugaidi, kutumia silaha na risasi za moto kinyume na sheria kutawanya mikusanyiko ya amani, kutumia magari yasiyo na namba za usajili, na kuwashikilia wanachama wa upinzani katika maeneo yasiyojulikana.
Ripoti inasisitiza kuwa matumizi ya silaha za moto yanapaswa kuwa hatua ya mwisho kabisa ili kuzuia vifo au majeraha makubwa, na inawataka wahusika wote wa ukiukwaji wa haki za binadamu kuwajibishwa kupitia uchunguzi huru na wa haki.