
Taarifa hizo ni kulingana na kitengo cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Shifa ambako miili yao imefikishwa. Israel inaendelea kutanua operesheni za kijeshi hasa katika jiji la Gaza ambako imewaamuru wakaazi wahame. Inafanya hivyo kwa madai kuwa inapambana kuwaondoa wanamgambo wa Hamas katika eneo hilo inaloamini kuwa ndiyo ngome yao kuu iliyosalia.
Jeshi la Israel limesema Jumamosi kwamba zaidi ya watu 250,000 wameshaondoka katika jiji la Gaza. Wakaazi hao wameelekea katika maeneo mengine ya ukanda huo tangu jeshi hilo ilipoongeza mashambulizi kwenye jiji hilo. Jumamosi asubuhi Israel ilisambaza vipeperushi magharibi mwa jiji hilo ikiwataka waondoke kwa usalama wao kabla ya kuendelea na mashambulizi.