Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ametaka maandalizi ya Michuano ya AFCON 2027 kuanza mara moja, akisisitiza kuanzishwa kwa mashindano ya michezo katika shule zote za msingi na sekondari nchini kama sehemu ya shamrashamra za kuelekea mashindano hayo makubwa yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda. Makonda ametoa kauli hiyo leo Januari 13, 2026 alipowasili katika Ofisi za Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, saa chache baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino.
Amesema mashindano ya shule yataongeza hamasa na morali kwa Watanzania kuipenda na kuishangilia Timu ya Taifa, huku yakichochea matokeo chanya na kuibua vipaji vipya vya michezo miongoni mwa vijana. Aidha, Waziri Makonda ameitaka Wizara kuandaa programu maalum itakayowawezesha walimu wa shule za msingi na sekondari wenye mapenzi na michezo kupata mafunzo ya kitaalamu, ili wahitimu vyuoni wakiwa na uwezo wa kugundua, kukuza na kuongoza vipaji vya watoto katika sekta ya michezo.
