Pugu Kazimzumbwi yaimarisha mapato serikaliniPugu Kazimzumbwi yaimarisha mapato serikalini

PWANI: HIFADHI ya Msitu wa Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi imeendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika kukuza sekta ya utalii nchini, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi, na kupelekea kuchangia kuimarika kwa mapato ya serikali pamoja na ukuaji wa pato la taifa.

Taarifa hiyo imetolewa na Muhifadhi Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kisarawe, Regina Mwakifuna, wakati wa mahojiano maalumu na Daily News Digital, ambapo amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu, hifadhi hiyo imefanikiwa kukusanya mapato zaidi ya Sh bilioni 1.9.

Amefafanua kuwa mapato ya hifadhi yamekuwa yakiongezeka kila mwaka. Kwa mfano, mwaka juzi hifadhi hiyo iliingiza takribani Sh milioni 151, mwaka jana ikaingiza Sh milioni 225, huku mwaka wa fedha uliomalizika hivi karibuni mapato yakifikia Sh milioni 252.

Aidha, kwa nusu ya mwaka wa fedha unaoendelea, hifadhi tayari imekusanya takribani Sh milioni 160, hali inayotoa matumaini ya kuvuka makusanyo ya mwaka uliopita.

“Kadri tunavyozidi kusonga mbele, mapato yanaendelea kuongezeka. Tuna imani kuwa mwaka wa fedha unaoendelea tutakusanya mapato makubwa zaidi kuliko miaka iliyopita,” amesema Mwakifuna.

Akizungumzia idadi ya watalii, Mwakifuna amesema hapo awali hifadhi hiyo ilikuwa ikitembelewa zaidi na watalii kutoka nje ya nchi kutokana na uelewa mdogo uliokuwepo miongoni mwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Hata hivyo, hali imebadilika kwa sasa, ambapo watalii wa ndani wamekuwa wakiongoza kwa idadi kubwa.

“Awali wageni wa nje ndio waliokuwa wanaongoza kutembelea hifadhi kwa sababu haikuwa imetangazwa vizuri na wazawa wengi walikuwa na dhana kuwa utalii ni kwa ajili ya wageni wa nje pekee. Kwa sasa, kupitia matangazo na elimu, Watanzania wameanza kupenda na kuthamini vivutio vyao,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa sasa, kwa mwezi mmoja, hifadhi hiyo hupokea takribani watalii wa ndani 1,000, huku watalii wa nje wakiwa kati ya 15 hadi 30 tu.

Kuhusu mipango ya maendeleo, Mwakifuna amesema hifadhi inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ili kuwahudumia watalii wote, hususan wenye mahitaji maalum. Mikakati hiyo ni pamoja na kuandaa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, kujenga na kuboresha nyumba za kulala wageni, maeneo ya kupikia, pamoja na kuhakikisha hifadhi inatangazwa ndani na nje ya nchi.

Aidha, amewahimiza Watanzania kuachana na dhana potofu kwamba utalii ni kwa ajili ya wageni kutoka nje au kwamba kwenda kutalii ni kupoteza fedha.

Ameeleza kuwa utalii unampa mtu fursa ya kupata uzoefu mbalimbali ikiwemo kuendesha mitumbwi, kuvua samaki, kulala kwenye hema (tenti), kushiriki shughuli za upandaji miti kuanzia mbegu hadi mti kukua, pamoja na kupika na kula pamoja kama familia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *