SERIKALI imeainisha mkakati mahsusi wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini, kwa kuweka kipaumbele katika utoaji wa leseni, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, masoko ya uhakika pamoja na maeneo yenye taarifa za utafiti.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameeleza hayo wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika leo Januari 15, 2025 jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amesema kuwa shughuli zote za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini zinatekelezwa kwa mujibu wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria ya Madini, Sura ya 123, kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini kwa tija na uendelevu.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa Sera na Sheria hizo umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya madini, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kuimarika kwa usimamizi, uwazi na uwajibikaji, hali iliyosababisha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kuongezeka kutoka sh bilioni 173.7 mwaka wa fedha 2012/13 hadi kufikia sh trilioni 1.071 mwaka 2024/25.

Waziri Mavunde amesema, Serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo yenye taarifa za utafiti na kuwapatia leseni za uchimbaji mdogo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Nyanhwale, Simanjiro, Mbogwe na Chunya, hatua inayolenga kuongeza tija, usalama na mapato yao.
Aidha, amesema Wizara ya Madini imeanzisha mkakati wa Mining For A Brighter Tomorrow (MBT) unaolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo katika nyanja za mitaji, teknolojia na taarifa za kijiolojia, ili waweze kujitegemea badala ya kutegemea wadhamini kutoka nje ya nchi.