DODOMA: RAIS Dk Samia Suluhu Hassan amesema kipaumbele kikuu katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 kitakuwa utumiaji wa gesi asilia, ambapo jitihada zitalenga ukamilishaji wa mradi wa gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) wa Dola bilioni 42, ambao utaiweka nchi katika soko la nishati duniani.
Dk Samia amefafanua taarifa hiyo leo Januari 15, alipozungumza na makamishna wakuu, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Wakati Dira 2050 ikielenga ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia ongezeko la tija katika kilimo na kuongeza thamani katika viwanda, pia Dk Samia ameongeza kuwa Serikali itazingatia ufunguzi wa fursa mpya za kiuchumi kupitia uchumi wa bluu, uchumi wa kijani, usafirishaji, na mazingira ya kidijitali.
“Kwa upande mwingine, nchi inaendeleza mazingira yanayovutia uwekezaji, ubunifu, na kuongeza thamani ya ndani katika sekta muhimu ya madini. Hatua zetu zitalenga kuendeleza uwekezaji unaohakikisha teknolojia za kesho, kusaidia mpito wa nishati safi duniani, kukuza viwanda, na kutoa faida za moja kwa moja kwa Watanzania,” amesema Dk Samia.
Aidha, Dk Samia amezialika serikali, sekta binafsi, na mashirika ya maendeleo kushirikiana nasi katika sekta hii muhimu, huku akiongeza kuwa Serikali yake imejizatiti kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji, uwazi, na ujumuishi.
“Ninafurahishwa na kuunga mkono kwa G20 ajenda ya madini muhimu. Tanzania inakubali kikamilifu mpango huu na ipo tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa kuhakikisha rasilimali hizi zinachangia teknolojia safi duniani na ukuaji jumuishi hapa nyumbani,” ameongeza Dk Samia
