Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda amesema Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS), unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni utaongeza wigo wa kodi na kusimamia usawa.
Kamishna Mwenda amesema hayo jijini Dar es Salaam Januari 15, 2026 akifungua mafunzo huo kwa washauri wa kodi na kampuni ukaguzi ambako amesema mfumo huo unakwenda kufanya maboresho makubwa kwa mifumo ya kodi za ndani iliyopo na kuleta mapinduzi katika ukusanyaji mapato.
Amesema IDRAS itasaidia kubaini na kuwabana wakwepa kodi na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya huku wakiwezesha biashara.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema nia ya Serikali ni kuona mifumo ya taasisi za Serikali inasomana ili kuongeza uwazi na uwajibikaji na TRA inatekeleza kwa vitendo kupitia mfumo huo.
Amesema kupitia IDRAS walipakodi watatoa risiti za EFD bila kutumia mashine na kupatiwa hati/cheti cha uthibitisho wa kutokuwa na madeni ya kodi (Tax Clearance), jambo linalorahisisha biashara.
Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za ndani, Alfred Mlegi amesema TRA inatoa mafunzo hayo kwa washauri wa kodi ili kuongeza uelewa kwa jamii na walipakodi kuhusu mfumo huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC), CPA Victoria Soka amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kushauri masuala ya kodi na kuwawezesha wateja wao kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa urahisi.
#StarTvUpdate